Serengeti Boys yaingia 'mtegoni'

19Mar 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Serengeti Boys yaingia 'mtegoni'

BAADA ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa) kuifungia Mali kujihusisha na mchezo huo, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), Bakari Shime, amesema kundi lao litakuwa gumu zaidi kutokana na kubakia na timu tatu.

Serengeti Boys.

Serengeti Boys imefuzu kushiriki fainali za vijana za Afrika na baada ya Mali kufungiwa, sasa Kundi B limebakia na timu tatu ambazo ni Tanzania, Angola na Niger.

Akizungumza na gazeti hili jana, Shime, alisema kuwa umakini unatakiwa kuongezeka zaidi kwa sababu idadi ya mechi zimepungua.
Shime alieleza kuwa ili timu iwe katika nafasi nzuri ya kusonga mbele bila 'presha', itatakiwa kushinda mechi yake ya kwanza.

"Timu zikiwa chache kuna faida na hasara, ugumu unaongezeka kwa sababu ili msiwe na presha mnatakiwa kushinda mechi ya kwanza halafu ukiingia mchezo wa pili unasaka sare au ushindi wowote, lakini ukifungwa, ni lazima nawe ushinde mechi inayofuata," alisema Shime.

Kabla ya kwenda katika fainali hizo, Serengeti Boys itacheza mechi mbalimbali za kirafiki za kimataifa dhidi ya Burundi, Rwanda zitakazofanyika mjini Bukoba, Kagera na baadaye kusafiri kwenda Cameroon kuweka kambi na kujipima na wenyeji wao.

Kundi A katika fainali hizo linaundwa na wenyeji Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.

Timu nne zitakazofanya vizuri katika fainali hizo zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), zitafuzu kucheza fainali za vijana za dunia ambazo zitafanyika baadaye mwaka huu huko India.

Habari Kubwa