Serengeti Boys yanusa Kombe la Dunia

19May 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Serengeti Boys yanusa Kombe la Dunia

TIMU ya soka ya Tanzania ya U-17 'Serengeti Boys' jana ilijiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya Afrika kwa vijana baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-1 kwenye mchezo dhidi ya Angola uliochezwa jana jioni nchini Gabon.

Ushindi huo mbali na kuiweka Serengeti Boys karibu kabisa na hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, lakini pia imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwenye fainali za vijana za Dunia zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini India.

Katika mchezo huo wa jana, Serengeti Boys ikiwa imetoka kupata suluhu kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa watetezi Mali, ilicheza soka safi na kuwapa wakati mgumu Angola.

Serengeti Boys ilichukua dakika tano tu kupata bao la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake Kelvin Naftal ambaye alifunga kwa kichwa akiungaisha krosi safi ya Hassan Juma.

Baada ya goli hilo, Serengeti Boys iliendelea kuutawala mchezo huku ikifanya mashambulizi mfululizo, lakini kasi ndogo ya washambuliaji ilishindwa kutumia nafasi vizuri.

Makosa ya safu ya ulinzi ya Serengeti Boys yaliipa nafasi Angola kusawazisha bao hilo kupitia kwa Pedro Agustino aliyeruka juu kuunganisha kwa kichwa mpira ambao awali ulionekana kutokuwa na madhara langoni mwa Serengeti.

Timu hizo zilienda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa upande wa Stars ambao waliishambulia Angola na juhudi zao zikazaa matunda katika dakika ya 68 wakati Hassan Juma alipoiandikia Serengeti bao la pili.

Kwa matokeo ya jana, Serengeti Boys sasa imefikisha pointi nne na itacheza mchezo wake wa mwisho Jumapili dhidi ya Niger na jana walikuwa wanasikilizia matokeo mengine katika kundi lao ambapo jana usiku Mali walicheza na Niger.

Habari Kubwa