Serikali na mkakati rafiki kuinua sanaa

03Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali na mkakati rafiki kuinua sanaa

Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji unaolenga kuinua tasnia ya sanaa nchini ili kuendana na ushindani wa soko la kimataifa, ameeleza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe

 

Dk. Mwakyembe aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania,  Joyce Fissoo, aliyemwakilisha katika uzinduzi wa kampuni ya filamu na muziki ya Starline Films ya jijini Dar es Salaam.

 

Aliipongeza menejimenti ya Starline Films ambayo inaongozwa na vijana wa Kitanzania kwa kazi nzuri za awali ambazo wamezifanya, kwani aliwahi kuitembelea miezi minne iliyopita na kuonyeshwa baadhi ya kazi na uwekezaji unaokidhi matakwa ya soko la kisasa. 

 

“Nimeambiwa asilimia 90 ya watendaji wa Starline Films ni vijana. Nimefurahi na nimefarijika kwa namna ambavyo vijana hawa wa Kitanzania walivyoweza kujitolea na kuendesha kampuni hii ya kisasa inayojihusisha na utayarishaji wa filamu, muziki pamoja na matangazo. Ni dhahiri, hatua hii imetokana na mazingira rafiki ya uwekezaji hususan kwa Watanzania, ambayo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Rais John Magufuli katika kuiboresha sekta ya sanaa nchini,” alisema Mwakyembe.

 

“Kwa niaba ya serikali, napenda kueleza kuwa tunaitambua kampuni hii kama kiwanda kinachochakata na kuzalisha kazi za sanaa ya muziki na filamu pamoja na matangazo. Hivyo, ni hatua nzuri ya kuunga mkono jitihada na dhamira ya Rais Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Niwahakikishie kuwa serikali inawaunga mkono kwa hatua hii na itawasaidia kwa kadiri iwezavyo katika kuhakikisha mnapiga hatua mbele, na kuwa hamasa kwa makampuni mengine kuiga mfano huu,” aliongeza.

 

Alitoa rai kwa makampuni nchini kuwaamini vijana wa Kitanzania waliowekeza katika ubora wa kazi na ubunifu, kuwapa kazi ili kuwaunga mkono na kuchangia maendeleo ya tasnia ya sanaa nchini ambayo inatoa mchango mkubwa wa ajira unaochangia katika juhudi za kulisogeza taifa katika uchumi wa kati.

 

Pia, aliwahakikishia wadau wa sanaa ya filamu na muziki kuwa serikali kupitia vyombo vyake itaendelea kupambana na wizi wa kazi za wasanii pamoja na aina zote za unyonyaji na kwamba ili kupata uhalali na ulinzi dhidi ya kazi zao na jasho lao, wasanii wote wanapaswa kuzingatia matakwa ya sheria kwa kusajiliwa na Bodi ya Filamu kwa waigizaji, na wasanii wote kwa ujumla kusajiliwa na kutambuliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Staline Films, Silver Oddo, aliishukuru serikali kwa kazi nzuri inayofanyika katika kurasimisha tasnia ya sanaa nchini pamoja na kusaidia kuhuisha mazingira bora ya uwekezaji, ulezi na usimamizi wa kazi za sanaa.

 

Habari Kubwa