Seseme, Shomary wasajiliwa Kagera

06Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Seseme, Shomary wasajiliwa Kagera

KATIKA kuhakikisha inakuwa imara na kurejea kwenye ushindani, uongozi wa Ligi Kuu Tanzania Bara umetangaza kuwasajili wachezaji watatu wapya kwa ajili ya msimu ujao, imeelezwa.

Ally Shomary wa Mtibwa Sugar

Nyota ambao wametangazwa kutua Kagera Sugar jana kuwa ni pamoja na Abdallah Seseme kutoka Mwadui FC ya mkoani Shinyanga, Ally Shomary wa Mtibwa Sugar na Zawadi Mauya ambaye alikuwa akiitumikia Lipuli FC ya Iringa.

Meneja wa Kagera Sugar, Mohammed Hussein, aliliambia gazeti hili kwamba wamejipanga "kukisuka" kikosi chao kwa sababu hawataki kuona wanaendelea kuwa kwenye wasiwasi wa kushuka daraja kama ilivyotokea kwa misimu mitatu iliyopita.

Hussein alisema kuwa licha ya kusajili wachezaji wa ndani tu, wanaamini Kagera Sugar itaendelea kutoa ushindani kwa klabu kongwe, lakini ikidhamiria kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

"Tumeshaanza kukisuka upya kikosi chetu, tunatarajia ushindani utaongezeka tena katika msimu unaokuja kama ambavyo inaonekana, kila timu inajiimarisha kwa sababu haitaki kuwa kibonde, tunasajili kulingana na mahitaji yetu na si kuangalia wengine wanafanya nini, tunaamini wachezaji hawa tunaowasajili, watasaidia kutimiza malengo yetu," alisema kiongozi huyo.

Aliwataja wachezaji wengine ambao waliwasajili tayari kuwa ni Evarist Mujwahuki kutoka Mbao FC ya jijini Mwanza, Erick Kyaruzi na Frank Ikobeki, wote kutoka Mbeya City.

Msimu uliomalizika, Kagera Sugar inayofundishwa na Mecky Maxime, ilinusurika kushuka daraja baada ya kuwafunga Pamba FC ya Mwanza mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano wa Play Off kufuatia sare ya bila kufungana katika mchezo wa kwanza.

Habari Kubwa