Sevilla kuleta neema Dar leo

21May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Sevilla kuleta neema Dar leo

WAKATI mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Europa League, Sevilla ya Hispania ambao wamemaliza msimu huu wa La Liga wakiwa nafasi ya sita, wakitarajiwa kuwasili nchini leo-

kwa ajili ya mechi ya kirafiki iliyoandaliwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa kwa ushirikiano na La Liga, neema kibao zinatarajiwa kupatikana katika ziara ya klabu hiyo.

Sevilla ambayo inatarajiwa kushuka Uwanja wa Taifa keshokutwa Alhamisi kuvaana na Simba kwenye mechi ya kirafiki, kabla ya mchezo huo itafanya shughuli mbalimbali za kuinua sekta ya michezo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, alisema SportPesa inakwenda kuweka historia kwa mara nyingine tena nchini kwenye sekta ya mpira wa miguu kwa kuileta timu ya Sevilla.

“Kupitia ujio wao timu ya Sevilla watafanya shughuli mbalimbali zenye lengo la kuinua sekta ya michezo nchini kwa vijana na mpira wa miguu kwa ujumla.

“Watatoa mafunzo ambayo yatahudhuriwa na timu ya vijana ya Bom Bom FC katika Uwanja wa Uhuru bila kusahau semina elekezi itakayotolewa na maofisa wa klabu ya Sevilla kwa viongozi wa klabu za hapa nchini, TFF na washirika wake ili wapate kuimarika kitaaluma na kupata uelewa jinsi ya kuongeza mapato ya klabu zao.

Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi aliwatangaza waamuzi watakaochezesha mechi hiyo kuwa ni mwamuzi wa kati, Elly Sasii akisaidiwa na Mohammed Mkono kutoka jijini Tanga na Soud Lila wa Dar es Salaam wakati Jonesia Rukyaa wa Kagera atakuwa mwamuzi wa akiba.

“Waamuzi wanaochezesha mchezo huu wote ni waamuzi wenye beji za Fifa, mchezo huu mbali ya kujitangaza kama nchi, lakini pia ni sehemu ya kutangaza vitu vyetu mbalimbali wakiwamo wachezaji na waamuzi,” alisema Madadi.

Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Haji Manara alisema bado wanaendelea kuwashukuru SportPesa kwa kufanikisha ujio wa Sevilla nchini, na ni fursa ambayo kila timu ya mpira wa miguu Afrika ingetamani kuipata.

“Maandalizi ya mechi na Sevilla yanaendelea vizuri, timu imeelekea Singida kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Singida United tarehe 21 (leo). Tunafahamu ukubwa wa mechi hii na tunawaahidi Wanasimba na Watanzania kwa ujumla kuwa tutatumia fursa hii kujitangaza kimataifa kama klabu, vilevile ni nafasi nzuri kwa wachezaji wetu kujitangaza na kujulikana kimataifa," alisema Manara.

Tiketi za mechi hiyo ya kirafiki zinapatikana kwenye vituo vyote vya mafuta vya Puma pamoja na vituo vyote vinavyotoa huduma ya Selcom kwa gharama ya kuanzia Sh. 5,000.

Habari Kubwa