Shekimweri ajipanga kuinyanyua Mpwapwa

27Jan 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe Jumapili
Shekimweri ajipanga kuinyanyua Mpwapwa

MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa jijini hapa, Jabir Shekimweri amesema anajipanga kusaidia kuendeleza na kuinua vipaji mbalimbali vya michezo vilivyomo katika wilaya yake.

MKUU WA WILAYA YA MPWAPWA JABIR SHEKIMWERI

Shekimweri alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa katika ziara maalum aliyoiandaa kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo ya michezo kwenye wilaya hiyo.

Alisema atahakikisha timu za Mpwapwa zinafanya vizuri hasa katika mchezo wa soka na hatimaye kuwapa nafasi vijana watangaze vipaji vyao.

"Napenda kuwa wazi, bado sijaridhishwa na hali ya uendeshaji wa mashindano mbalimbali yanayofanyika katika wilaya hii, mashindano mengi yamekuwa hayana ubora, tunahitaji kuongeza nguvu katika jambo hili," alisema Shekimweri.

Aliongeza kuwa watu wa Mpwapwa wanapenda kufanya mazoezi, lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa viwanja, hivyo chini ya uongozi wake watahakikisha tatizo hilo linamalizika.

Aliahidi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa wilaya hiyo, atajenga "gym" ya kisasa ili watu wafanye mazoezi kwa uhuru na amani.

 

 

Habari Kubwa