Shime atoa siri ya mafanikio Tanzanite

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Shime atoa siri ya mafanikio Tanzanite

MABINGWA wapya wa michuano ya Cosafa U-20 kwa upande wa wanawake, timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania chini ya miaka 20 (Tanzanite), wamerejea jana jijiini Dar es Salaam na kombe hilo huku wakianika siri kubwa ya mafanikio yao.

Tanzanite ambayo katika mechi ya fainali iliyopigwa Uwanja wa Wolfson juzi  ililipa kisasi kwa kuifunga Zambia mabao 2-1, idadi kama iliyofungwa awali na Wazambia hao kwenye hatua ya makundi, imetwaa ubingwa huo huku ikiwa imepoteza mchezo mmoja tu katika mashindano hayo.

Kocha Mkuu wa Tanzanite, Bakari Shime, aliliambia Nipashe kuwa siri kubwa ya mafanikio hayo ni kujiamini na kucheza soka la kushambulia mwanzo mwisho.

"Kazi ilikuwa moja tu, kutafuta matokeo na kulipa kisasi kwa wapinzani wetu kwa kuwa tuliingia uwanjani na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 mchezo wa hatua ya makundi.

"Wachezaji walionyesha juhudi na mbinu kubwa ilikuwa ni kushambulia mwanzo mwisho jambo ambalo limesaidia timu kutwaa ubingwa, shukrani kwa mashabiki kwa sapoti kubwa," alisema Shime.

Tanzanite imerejea nchini ikitokea Port Elizabeth, Afrika Kusini ilipokua ikishiriki mashindano hayo ambapo imefanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa kuonyesha soka la kuvutia na kiushindani.

Katika hatua ya makundi, Tanzanite ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana, 8-0 dhidi ya Eswatini na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya  Zambia kwa kuchapwa 2-1.

Baada ya hapo ilipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye nusu fainali dhidi ya Afrika Kusini kabla ya kuifunga Zambia 2-1 katika mchezo wa fainali iliochezwa juzi.

Mbali na Tanzanite kutwaa kombe hilo na medali za dhahabu, nahodha wa kikosi hicho, Enekia Kasonga alitangazwa kuwa mchezaji Bora wa Mashindano.

Habari Kubwa