Silaha Simba hazikamatiki

19Jul 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Silaha Simba hazikamatiki
  • ***Kocha afunguka bado hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba katika...

WAKATI wachezaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakifanya mazoezi ya aina mbalimbali ili kujiimarisha, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, amesema kuwa bado hakuna mchezaji mwenye uhakika wa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems,.

Kikosi hicho kimekuwa kikifanya mazoezi ya viungo "gym", uwanjani wakiwa na mipira na wakati mwingine bila ya kuchezea mipira.

Nyota hao ambao walianza kambi hiyo iliyoko kwenye mji wa Rustenburg nchini humo Afrika Kusini, wamekuwa wakitumia vifaa vya kisasa ambavyo vinatumiwa na timu zilizoendelea katika mataifa ya Ulaya, wakati wa maandalizi ya msimu mpya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aussems, alisema kuwa kila mchezaji wa Simba anaonyesha bidii kwenye mazoezi yanayoendelea kwa sababu anataka kujihakikishia nafasi kwenye kikosi hicho.

Aussems, ambaye msimu uliopita aliipeleka Simba katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema kwamba anafurahia kuona hali hiyo na kingine ni ukaribu wa wachezaji wake wapya na wa zamani, jambo ambalo alitarajia lingechukua muda.

"Tuna siku chache tangu tuanze mazoezi, na kumbuka tumekuja kwa makundi tofauti, lakini ukiwaangalia wachezaji, huoni tofauti, kila mmoja anafanya vema katika kila zoezi analoambiwa kufanya, tuko kama kundi, tunafanya kila kitu kinachotakiwa, ili tukitoka hapa tuwe imara na tayari kushindana," alisema Aussems.

Mbelgiji huyo aliongeza kuwa anaamini baada ya kupata mechi za kujipima nguvu, ndiyo atapata "picha" ya kikosi chake cha kwanza kitakavyokuwa.

Naye Mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally, aliliambia gazeti hili kwamba wachezaji wote ni wazima na wanafurahia mazingira ya kambo yao.

"Wachezaji wote wako salama, viongozi pia tuko sawa, tunaendelea kukamilisha mazungumzo na kati ya siku mbili hizi, tutafahamu tunaanza kucheza na timu ipi, bado pia tunaiweka miili tayari kukabiliana na ushindani," Ally alisema.

Taarifa nyingine kutoka Simba zinasema kuwa tayari klabu hiyo imeshapata vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini vya wachezaji wake wote wapya wa kimataifa ambao imewasajili.

Simba itaanza kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza dhidi ya JKT Tanzania, Agosti 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini wakati Yanga yenyewe itaanza kampeni zake Agosti 28 dhidi ya Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani.

Habari Kubwa