Simba ‘yakolea’ kwa straika wa Yanga

09May 2016
Somoe Ng'itu
Lete Raha
Simba ‘yakolea’ kwa straika wa Yanga

SIMBA SC inafikiria kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Yanga B, Atupele Green ambaye kwa sasa anachezea Ndanda FC ya Mtwara.

Mchezaji Atupele Green

Atupele mwenye kipaji cha kufunga ambaye alicheza pamoja na akina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu katika timu za vijana nchini, ni mongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwa kwenye rada za Wekundu wa Msimbazi.

Habari kutoka ndani ya Simba SC zimesema kwamba timu hiyo imevutiwa na Atupele baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu tangu aondoke Yanga mwaka 2009.

Na kishawishi kikubwa kwa uongozi wa Simba juu ya kusajiliwa kwa mchezaji huyo ni kocha Mganda, Jackson Mayanja ambaye amewahi kufanya kazi na mpachika mabao huyo katika timu ya Kagera Sugar ya Bukoba.

Mwenekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alipotafutwa kuzungumzia habari hizo alisema; “Ni mapema mno kuanza kuzungumzia usajili kwa sasa, hata ligi yenyewe hatujamaliza,”.

Wakati huo huo:Simba SC inashuka dimbani leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Simba SC inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kuendelea kuweka hai matumaini ya ubingwa unaowaniwa pia na Yanga SC, huku Azam FC ikiwa imekwishajifuta kwenye mbio hizo.

Simba SC ina pointi 58 baada ya kucheza mechi 26 na inaweza kufikisha pointi 70 ikishinda zake zote nne zilizobaki kuanzia wa leo dhidi ya Mwadui FC – maana yake bado ina nafasi ya kuwapiku vinara, Yanga wenye pointi 68 sasa baada ya kucheza mechi 27 katika mbio za taji la Ligi Kuu.

Mwadui FC yenye pointi 37 za mechi 27, yenyewe haimo kwenye mbio za ubingwa wala hofu ya kushuka, kwani tayari kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amekwishaiweka sehemu salama timu yake.

Habari Kubwa