Simba, Al Ahly dk. 90 kuamua

23Feb 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Al Ahly dk. 90 kuamua

VITA kamili ya Wawakilishi wa Tanzania katika mechi ya Kundi A ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji Simba dhidi ya Al Ahly kutoka Misri inatarajiwa kufanyika leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

***Matola, Bocco waahidi watafanya kila njia ili kuendeleza ubabe nyumbani...

Simba itawakaribisha vigogo hao wa Afrika ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini katika mechi yake ya kwanza ya Kundi A dhidi ya AS Vita ya Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ni mechi ambayo inatarajia kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka barani Afrika, ambao macho na masikio yao yataelekezwa Tanzania kuangalia nini kitatokea baina ya timu hizo mbili.

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola amekiri mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu wanaocheza wote ni mabingwa, lakini wamejipanga kufanya kila njia ili kupata ushindi nyumbani.

"Siyo mechi rahisi. Hii ni Ligi ya Mabingwa, lakini tumejipanga. Tunakutana na timu nzuri, kubwa na bora zaidi, lakini tumejipanga kupata ushindi. Ninachoweza kuwaambia Watanzania hatuna majeruhi hata mmoja, hili ndilo tunalojivunia, hivyo tuna uwanja mpana wa kuchagua kikosi chetu kwa ajili ya kupambania ushindi," alisema Matola.

Nahodha na mshambuliaji wa timu hiyo, John Bocco ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu na sasa yuko fiti, alisema kikosi chao kimejipanga vyema kuondoka na ushindi, licha ya kwamba wanawaheshimu wapinzani wao.

"Tumejipanga vizuri, tunakwenda kucheza tukiwa na morali, tunawaheshimu wapinzani, ni wazoefu na ni wakubwa Afrika, lakini tunaamini mbinu tulizozipata kutoka kwa walimu wetu, Bocco alisema.

Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pisto Mosimane, alisema wanakumbuka kipigo walichokipata kwenye mechi ya mwaka 2019, hivyo wamefanyia kazi makosa waliyoyafanya na wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa.

"Ni kweli, waliwahi kutufunga kwenye uwanja wao wa nyumbani, yale makosa tumeyafanyia kazi, tutaingia uwanjani kwa juhudi za kusaka ushindi," alisema Mosimane.

Hata hivyo kocha huyo amelalamikia hali ya joto ya Dar es Salaam, na kusema pamoja na mazingira hayo, wapinzani wao wako vizuri na wao watapambana kupata matokeo mazuri.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye uwanja huo ilikuwa ni Februari 12, mwaka juzi, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi ambapo Simba ilishinda bao 1-0, shukrani kwa mshambuliaji wake Mnyarwanda Meddie Kagere ambaye bado yupo kwenye kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Hata hivyo, Simba itakuwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 5-0 kwenye mechi ya kwanza ya kundi hilo, iliyochezwa Februari 2, mwaka 2019, nchini Misri.

Itakuwa ni mara ya tano kwa Simba kukutana na Al Ahly kwenye historia ya timu hizo, kwani zimeshakutana mara nne, huku kila timu ikishinda nyumbani kwake, Ila maana Simba haijawahi kufungwa au kutoa sare na Wamisri hao wakiwa kwenye ardhi ya Tanzania.

Mara ya kwanza zilikutana mwaka 1985  kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika nchini Tanzania kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Simba ikishinda mabao 2-1, ya Zamoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani, Mohamed Al Khatib 'Bibo' akiifungia bao la kufutia machozi, Al Ahly wakiwa ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo.

Mara ya mwisho Simba kupoteza mechi ya kimataifa kwenye ardhi ya nyumbani ni miaka saba iliyopita. Ilikuwa ni Februari 17, 2013, ilipochapwa bao 1-0 dhidi ya Recreativo do Libolo ya Angola, ikiwa ni katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Al Ahly ndio wanaongoza katika msimamo wa Kundi A wakifuatiwa na Simba, AS Vita na El Merreikh ya Sudan ambayo ilichapwa mabao 3-0 katika mechi yake ya kwanza.

Habari Kubwa