Simba, Azam FC mechi ya kisasi

23Oct 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Azam FC mechi ya kisasi

MUDA utaongea! Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatarajia kuwakabili Azam FC katika mechi ya ligi hiyo itakayochezwa leo kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba itashuka uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-2, walioupata katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii iliyochezwa mapema Agosti mwaka huu.

Akizungumza jana jijini, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani kutokana na kila kikosi kuundwa na wachezaji wenye uwezo na uzoefu katika ligi hiyo.

Aussems alisema kuwa amewaandaa vema wachezaji wake na kuwakumbusha kuongeza utulivu wanapokuwa na mpira ili waweze kutawala mchezo huo na hatimaye kufunga mabao.

"Tumefanya maandalizi mazuri, tunaifahamu Azam, wanatufahamu, kwa ujumla niseme tuko tayari kwa mchezo huo, ni mchezo muhimu na unaotarajiwa kuwa ushindani, si mechi rahisi," alisema Aussems.

Naye Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema kuwa wako tayari kwa mchezo huo na wamejiandaa kuendeleza kasi ya ushindi.

"Lengo letu ni kupata pointi tatu, tunajua Azam ni timu nzuri, yenye uzoefu na yenye uwezo, ila hii haitufanyi tuwe na hofu, tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema meneja huyo.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche, amesema kuwa kikosi chake hakina hofu na kitaingia uwanjani kwa lengo moja la kupambana kusaka ushindi katika mchezo huo muhimu.

Cheche alisema kuwa kikosi chake hakina mchezaji ambaye ni majeruhi na amewataka mashabiki wao kujaa kwa wingi ili kuwaongezea morari ya kupata matokeo mazuri.

Simba itaingia katika mechi hiyo bila ya kupata huduma kutoka kwa nahodha wake, John Bocco wakati wachezaji wa Azam waliokuwa majeruhi, akiwamo Suleiman Ndikumana, Donald Ngoma na beki, Aggrey Moriss wamerejea kikosini wakiwa imara.

Habari Kubwa