Simba, Azam FC zaidi ya heshima

01Jul 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Azam FC zaidi ya heshima
  • Zinakutana katika mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA, zikitambiana...

HAKUNA kulala! Ni pale mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba watakapowakabili Azam FC katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA itakayochezwa leo kuanzia 1: 00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Azam FC ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ambayo hutoa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba itashuka dimbani leo tayari ikiwa na tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na mechi sita mkononi za kumaliza msimu wa 2019/20, huku Azam FC yenyewe zikipambana na Yanga kumaliza kwenye nafasi ya pili.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kikosi chake kiko tayari na mechi ya leo na wamejipanga kuendelea kupambana ili kutimiza malengo ya kukinyakua kikombe cha mashindano hayo.

Sven alisema anafahamu mechi hiyo itakuwa ngumu na yenye ushindani, lakini amewaandaa wachezaji wake kucheza katika kiwango bora kwa sababu Azam FC pia ni timu nzuri na yenye wachezaji wazoefu.

"Tunachokiangalia ni kufanya vizuri, mechi haitakuwa rahisi, lakini tunacheza na timu ambayo kila kitu chake kinategemea michuano hii, kwa kifupi tuko tayari kwa mapambano," alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Aliongeza baada ya kumaliza kukamilisha malengo namba moja, nguvu zao wamezielekeza kwenye michuano hii ambayo msimu huu wanahitaji kuweka rekodi nzuri na si kutolewa mapema.

Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alisema amewaandaa wachezaji wake kupambana na kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili wasonge mbele katika michuano hiyo.

"Ni mechi kubwa, kimahesabu tayari Simba ni mabingwa, nawapongeza pia kwa kutwaa ubingwa, wana wachezaji wazuri na kila nafasi ina wachezaji wawili wazuri, lakini kesho (leo), naamini haitakuwa siku yao, tutaingia uwanjani kwa lengo la kushinda," alisema Cioaba.

Alieleza leo wachezaji wake wanatakiwa kucheza soka la kuvutia, wachezaji wake kuelewana na kuwa na ari ya juu na kuongeza umakini kila watakapokuwa na mpira.

"Wanatakiwa kujitoa zaidi, kwa sababu ni mchezo ambao timu moja itatoka na timu nyingine itaendelea na mashindano, najua kesho (leo), ni siku muhimu na ninawakumbusha wachezaji wangu kuongeza umakini katika kufunga, huu ndio ujumbe kwa mastraika wangu," alisema kocha huyo.

Kiungo wa timu hiyo, Frank Domayo, aliliambia gazeti hili mechi ya leo itakuwa ngumu kwa pande zote, lakini wao watashuka dimbani kupambana kusaka ushindi.

"Simba ni timu ngumu, inawachezaji wazuri, kila kitu kiko sawa, na sisi pia tuna nafasi, kikubwa ni kupambana kuwania pointi tatu, kikosi kiko imara, tumekaa pamoja kama wachezaji na kuelezana malengo yetu, " Domayo alisema.

Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC, ambayo leo itaendelea kuwakosa nyota wake wa kimataifa kutoka Ghana, akiwamo golikipa Razack Abalora.

Robo fainali nyingine ya michuano hiyo itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Sahare All Stars ya jijini Tanga dhidi ya Ndanda FC kutoka mkoani Mtwara.

Habari Kubwa