Simba, Azam vitani Ligi Kuu

21Nov 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Azam vitani Ligi Kuu
  • ***Kila timu yatamba kusaka ushindi ili kujiimarisha kwenye msimamo wa...

SAFARI ya kuwania pointi tatu muhimu inatarajia kuendelea kwa mabingwa watetezi, Simba kukabiliana na Coastal Union ya Tanga katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha.

Coastal Union imelazimika kuhamia Arusha baada ya Uwanja wake wa CCM Mkwakwani kufungwa kutokana na kutokidhi sifa zilizowekwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, aliliambia gazeti hili kikosi chake kilifika salama jijini Arusha na kiko tayari kwa mchezo wa leo.

Sven alisema amejiandaa vyema kukutana na ushindani katika mchezo huo kwa sababu kwao, mabingwa watetezi, michezo yote ni migumu.

Kocha huyo alisema anahitaji kupata ushindi katika mechi ya leo ili kujiimarisha kwenye mbio za kutetea taji hilo wanalolishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.

"Tunatarajia kukutana na ushindani, mechi haitakuwa nyepesi, kila timu imejipanga kufanya vizuri na zaidi inapokutana na sisi, tutaingia kwa tahadhari na tuko tayari kwa mapambano," alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Coastal Union, alisema kikosi chake kimejiandaa kuwashangaza mabingwa hao watetezi kwa kuchukua pointi zote katika mechi hiyo.

Mgunda alisema kama wachezaji wake watatulia na kuongeza umakini, anaamini ataifunga Simba na kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa.

"Tuko tayari kwa mchezo, ni mchezo ambao unahusisha wachezaji wanaojuana, kikubwa ni kuongeza umakini, mpira unapokosea unampa nafasi mpinzani wako kukuadhibu, hatutaki hilo litokee katika mechi hii," Mgunda alisema.

Naye Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, alisema wamejiandaa vizuri kuekelea mchezo wao dhidi ya KMC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Aliwataja wachezaji watakaokosekana katika mechi hiyo ambao ni majeruhi ni pamoja na kiungo, Salum Aboubakar 'Sure Boy', beki, Oscar Masai na Frank Domayo ambaye aliumia kwenye mazoezi ya jana.

Aliongeza wanatarajia kukutana na ushindani katika mchezo huo kutokana na rekodi nzuri ya KMC inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Kaimu Kocha Mkuu wa KMC, John Simkoko ametamba timu yake itaibuka na ushindi katika mechi hiyo.

"Katika mchezo wa kesho (leo), hakuna cha pira Ice cream, strawbery wala pira mkate, KMC itakwenda kuonyesha pira spana, tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu yao, kikosi chetu ni kizuri hivyo Azam wajipange, wasije kutoa sababu pindi watakapofungwa," Simkoko alisema.

Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya Polisi Tanzania dhidi ya Ihefu FC wakati JKT Tanzania watawakaribisha Gwambina kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma.

Habari Kubwa