SIMBA BABA LAO

13Jul 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
SIMBA BABA LAO
  • Yaichapa Yanga mabao 4-1 na kuzima ndoto zao za kushiriki michuano ya CAF, Namungo haooo...

WAMELIPA Kisasi! Simba imeendelea kung'aa baada ya kufanikiwa kuifunga Yanga mabao 4-1 katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA iliyochezwa jana jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Mbali na kutoa kichapo, Simba imeinyima Yanga tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao, na hivyo sasa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara watakutana na Namungo katika fainali itakayochezwa Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mbrazil Gerson Fraga ndiye aliifungia Simba bao la kwanza katika mchezo huo baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Clatous Chama ambaye kabla ya kutoa pasi, aliwazungusha wachezaji wawili wa Yanga, Said Makapu na Papy Tshishimbi.

Bao hilo lilidumu mpaka timu hizo zilipokwenda mapumziko katika mchezo huo uliokuwa na kasi pamoja na ubabe kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili.

Chama ambaye alikuwa katika kiwango chake jana, alifunga bao la pili baada ya kuanzisha shambulizi na kumpatia Bocco, halafu nahodha huyo akamrejeshea mfungaji huyo dakika ya 48 ya mchezo huo.

Simba ikiendeleza ubora wake ilipata bao la tatu kupitia kwa Luis Miquesson ambaye aliwahi mpira wa kichwa uliookolewa na Tshishimbi ambaye alikuwa anaondoa hatari kwenye lango la timu yake dakika ya 51.

Kiungo Muzamiru Yassin aliyeingia akichukua nafasi ya Fraga alimalizia mpira uliotemwa na Menatha ambaye alishindwa kudaka shuti la Meddie Kagere na hivyo kuiandikia Simba bao la nne ambalo liliwanyamazisha mashabiki wa Yanga waliokuwa wanaamini wanaweza kupindua matokeo.

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi katika lango la Simba kupitia kwa David Molinga, lakini beki wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kennedy Juma aliwahi kuruka na kuokoa shambulizi hilo kwa kichwa na mpira kwenda nje dakika ya nne.

Simba walijibu shambulizi hilo dakika mbili baadaye kwa kufanya kashikashi katika lango la wapinzani wao, lakini golikipa wa Yanga, Menata Mnacha alikuwa makini kwa kupangua shuti kali lililopigwa na kiungo, Jonas Mkude.

Dakika ya sita, winga hatari wa Simba alipoteza nafasi ya kufunga baada ya kupiga juu ya lango na kupoteza pasi aliyopewa na Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr'.

Nahodha wa Simba, John Bocco alimpa pasi fupi Chama lakini Mzambia huyo aliinyima Simba nafasi ya kupata bao la mapema baada ya shuti alilopiga kupaa juu, huku tayari mabeki wa Yanga wamemwacha huru kufanya shambulizi hilo ndani ya eneo la hatari huku Bocco naye akikosa goli kwa kupiga pembeni dakika ya 31.

Aishi Manula 'Tanzania One' aliinyima Yanga nafasi ya kusawazisha baada ya krosi nzuri aliyopiga iliyokuwa inaelekea langoni kuishia mikononi mwa Tanzania One huyo dakika ya 34 huku Lamine Moro akiokoa hatari nyingine langoni mwao kupitia mpira uliopigwa na Miquissone.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein 'Zimbwe Jr', Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Gerson Fraga/ Muzamiru Yassin (dk 80), John Bocco/ Meddie Kagere (dk 73), Clatous Chama na Francis Kahata/ Hassan Dilunga (dk73).

Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffari Mohammed, Said Makapu, Lamine Moro, Papy Tshishimbi/ Nchimbi (dk 55), Deus Kaseke, Feisal Salum, Haruna Niyonzima/ Kelvin Yondani (dk 55), David Molinga na Bernard Morrison/ Patrick Sibomana (dk 64).

 

YANGA YATANGULIA

Saa 9: 02 mchana; Kikosi cha Yanga kilikuwa cha kwanza kuingia uwanjani kwa kutumia gari mbili aina ya Coaster huku basi lao kubwa lililozoeleka likiingia tupu.

Dereva wa Yanga aliingia na basi hilo akiwa peke yake na kwenda kuliweka kwenye sehemu maalumu ya maegesho.

9:18 mchana; Kikosi cha Simba kilitinga kwenye uwanja huo wa kisasa nchini kikiwa kwenye busi lao na wachezaji wake wote pamoja na benchi la ufundi.

Licha ya serikali kutangaza kuuza tiketi chache ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, mashabiki wa Simba waliendelea kuwa wengi zaidi uwanjani hapo wakiwa wamevalia jezi za rangi nyekundu na nyeupe.

Habari Kubwa