Simba, Biashara hesabu zitaongea

16Sep 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Biashara hesabu zitaongea

WAKATI kikosi cha Simba kikianza mazoezi kuikabili Biashara United, kila upande unatabiri mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam utakuwa wenye ushindani.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliliambia gazeti hili kikosi chake kimeanza kujiimarisha kuelekea mchezo huo na lengo ni kurekebisha makosa yaliyotokea katika mechi iliyopita.

"Mpira ni mchezo wa makosa, tumeshafunga hesabu za mechi iliyopita, sasa tunajiandaa kuikabili Biashara, akili zetu ni kuona tunapambana kusaka ushindi," alisema Rweyemamu.

Naye Kocha Mkuu wa Biashara United, Francis Baraza, alisema mechi dhidi ya Simba itakuwa ngumu kwa sababu wanacheza na timu yenye kibarua kimoja cha kutetea ubingwa wanaoushikilia.

Baraza alisema wataingia uwanjani kwa  kuwaheshimu, lakini wakiwa na lengo la kutafuta alama muhimu katika mchezo huo wa raundi ya tatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo alisema licha ya kupata ushindi katika michezo yao miwili iliyopita, hawatabweteka na ataendelea kupanga mbinu zaidi za ushindi dhidi ya vigogo hao wa soka nchini.

Alieleza maandalizi ya mechi hiyo yatakuwa tofauti na jinsi alivyocheza mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Gwambina na Mwadui FC, kwa sababu ya aina ya wachezaji wanaotarajia kukutana nao.

“Mechi hiyo ni ngumu, hatuwaogopi ila ninawaheshimu. Watu wanatakiwa watambue tunaenda kucheza na mabingwa, lazima uwape heshima yao, ukizingatia ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri ambao wanaweza kumpa kocha matokeo wakati wowote wanapoamua kucheza," Baraza alisema.

Alisema bado anaendelea kukijenga kikosi chake na amezitumia mechi mbili zilizopita kama sehemu ya kuimarisha wachezaji wake kuelekea mchezo huo dhidi ya Simba.

Habari Kubwa