Simba bingwa aliyestahili

22May 2019
Adam Fungamwango
DAR
Nipashe
Simba bingwa aliyestahili
  • ***Aussems aogeshwa uwanjani, sherehe Singida hadi Dar wakiiwahi Sevilla Taifa kesho huku...

HATIMAYE Simba imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara, huku ikiweka rekodi ya kulitwaa taji hilo ikiwa ardhi ya Singida kwa mara ya pili mfululizo.

Wachezaji wa Simba wakishangilia kwa staili yao ya mabingwa, wakati walipoichapa Ndanda FC mabao 2-0 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Jumapili.

Ilikuwa ni shangwe, nderemo, hoi hoi na furaha kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida jana kwa wanachama, wapenzi, mashabiki, viongozi, wachezaji na makocha wa Klabu ya Simba, baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, ilipoichapa Singida United mabao 2-0 huku Kocha Mkuu, Patrick Aussems akiogeshwa kwa maji na wachezaji wake kwa furaha ya ubingwa.

Huu unakuwa ni ubingwa wa 20 kwa Simba na kuendelea kuwa timu ya pili kutwaa ubingwa mara nyingi, nyuma ya Yanga ambayo imeutwaa mara 27.

Simba ambayo tangu kuanza kwa msimu huu ilionekana kustahili ubingwa huo kutokana na usajili makini iliyoufanya na hatimaye kuonyesha kiwango mwanzo mwisho, ilikuwa ikihitaji pointi mbili tu kuweza kufikisha alama 90 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ile, lakini kwa ushindi huo imefikisha jumla ya pointi 91.

Mabao kupitia kwa Meddie Kagere aliyetupia la 23 msimu huu na lile la kipindi cha pili la nahodha John Bocco (la 16 kwake), yalitosha kuihakikishia Simba inatwaa ubingwa huo msimu huu huku ikiwa na mechi mbili mkononi kufuatia kufikisha pointi 91 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika msimamo wa ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Mei 28, mwaka huu ikishirikisha timu 20.

Simba ambayo msimu uliopita ilitwaa ubingwa huo katika Uwanja wa Namfua baada ya kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Singida United, sasa inarejea jijini Dar es Salaam kushuka Uwanja wa Taifa kesho kuivaa Sevilla ya Hispania kwenye mechi ya kirafiki iliyoandaliwa na wadhamini wao Kampuni ya SportPesa kwa kushirikiana na La Liga.

Kagere alifunga bao hilo dakika ya tisa tu ya mchezo, baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Singida United. Shambulizi hilo lilikuwa ni la kujibu lile la dakika ya nne wakati Boniface Maganga aliukuta mpira uliokosewa na Nicolaus Gyan na kupiga suti lililotoka pembeni kidogo mwa goli.

Baada ya bao hilo kulikuwa na kosakosa za hapa na pale hadi zilipomalizika dakika 45 za kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili kilipoanza, Singida walifanya mashambulizi mawili hatari ambayo nusura yawapatie bao, lakini washambuliaji wao kina Habib Kyombo na Geofrey Mwashiuya waliponasa mpira hawakuwa makini.

Huku Uwanja wa Namfua ukiwa umefurika mashabiki, Simba ilifanikiwa kupata bao la pili lililofungwa kwa kichwa na Bocco.

Bocco alifunga bao hilo dakika ya 61 wakati kipa wa Singida, Said Lubawa akiwa nje ya uwanja baada ya kushindwa kurejea kwa kuumia. Kipa huyo aliufuata mpira aliorudishiwa na beki wake ulioonekana kama unataka kutoka na kuwa kona, aliukimbilia na kuupiga nje, lakini mwenyewe pia akiutoa nje.

Kilichofanyika kwa wachezaji wa Simba, ulirushwa mpira kwa Emmanuel Okwi ambaye alipiga krosi haraka, huku golini kukiwa na mabeki wa Singida na Bocco aliruka juu na kuukwamisha wavuni kwa kichwa.

Habari Kubwa