Simba bingwa FA

26Jul 2021
Na Waandishi Wetu
Kigoma
Nipashe
Simba bingwa FA
  • …Yalipa kisasi kwa watani zao wakati Tonombe akiipa pancha Yanga kwa kulimwa kadi nyekundu…

BAO pekee lililofungwa na Mganda, Thadeo Lwanga jana liliifanya Simba kulipiza kisasi cha kufungwa Julai 3, kwenye mechi ya Ligi Kuu, kwa kuwatwanga watani zao wa jadi Yanga bao 1-0 na kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania, maarufu kama FA, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma jana.

Lwanga aliunganisha mpira kwa kichwa kwa kona iliyopigwa na Luis Miquissone na mpira ukawapita mabeki wa Yanga na kipa wao, ukajaa wavuni.

Ushindi wa Simba dhidi ya Yanga umeifanya timu hiyo kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo, lakini kuwafunga tena mara ya pili watani wao wa jadi kwenye michuano hiyo.

Ikumbukwe Simba iliifunga Yanga mabao 4-1 kwenye mechi ya nusu fainali Julai 12, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Yanga walianza kwa kasi, kwani mpira ulipoanza tu ilipigwa pasi ndefu kwa Tuisila Kisinda ambaye alikimbia kwa kasi na kupiga krosi iliyokosa muunganishaji, sekunde ya 30.

Dakika ya pili, golikipa wa Simba, Aishi Manula aligongana na Ditram Nchimbi kutokana na shambulizi kali langoni mwake dakika hizo za mwanzoni.

Hatimaye Simba ilifika golini kwa Yanga dakika ya 30, baada ya Miquissone kuukimbilia mpira ulioonekana kama unataka kutoka na kupiga krosi iliyomkuta Chris Mugalu akapiga 'tik-tak' ambayo iliwagonga mabeki wa Yanga na kurejea uwanjani.

Dakika sita baadaye Miquissone alikuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, lakini shuti lake lilimbabatiza Bakari Mwamnyeto na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kiungo mkabaji wa Yanga, Mukoko Tonombe alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Ahmed Aragija dakika ya 45, baada ya kumpiga kiwiko nahodha wa Simba, John Bocco.

Kipindi cha kwanza timu zote zilionekana kucheza mchezo wa pasi ndefu, huku wachezaji wa timu zote mbili wakiwa hawajatulia.

Pia Uwanja wa Lake Tanganyika ulionekana kama mdogo kutokana na mara kwa mara pasi za wachezaji wa timu zote mbili kutoka nje.

Kipindi cha pili Simba iliingia kwa spidi kali na ilikuwa dakika 52, Miquissone alipaisha mpira akiwa kwenye nafasi nzuri baada ya kupewa pasi ya Mugalu.

Yanga nusura ipate bao dakika ya 62 kutokana na shambulizi la kushtukiza, baada ya Yacouba Songne kuupata mpira na kuwalamba chenga mabeki wa Simba, kabla ya kuachia shuti kali lililotoka juu, nje kidogo ya lango.

Mugalu naye aliikosesha Simba bao dakika ya 72, akiwa ana kwa ana na kipa Farouk Shikalo alipopiga shuti lililombabatiza na kutoa kona.

Lwanga, baada ya kukosa bao dakika ya 70, alisawazisha makosa yake kwenye dakika ya 79 na kupeleka furaha Msimbazi.

Pamoja na timu zote kufanya mabadiliko kwa nyakati tofauti, lakini Simba ilifanikiwa kulilinda goli lake kwa dakika 11 zilizobaki.

KURUSHIANA CHUPA

Baada ya bao kulikuwa na vita vya kurushiana chupa za maji kati ya mashabiki wa Yanga na Simba.

Na baadhi ya mashabiki wa Yanga wakaamua kuondoka katika jukwaa lao na kwenda nje huku wakisusia mechi.

FISTON AVULIWA SOKSI

Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Abdoul alivuliwa soksi na mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la timu yake hiyo, kwa sababu alivaa za rangi nyekundu akiwa tofauti na wachezaji wenzake walivalia rangi nyeusi na njano.

Kitendo hiko kilifanyika muda mfupi wakati vikosi vya timu zote mbili vikiwa uwanjani vinafanya mazoezi mepesi kabla ya kuanza kwa mchezo huo.

TIMU KUWASILI

Kikosi cha Simba kiliingia uwanjani saa 8:28 kikiambatana na viongozi wote na baada ya dakika 5 kikosi cha Yanga kiliingia kupitia geti la mashabiki na kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Hadi saa 6:46 na 7:47 mchana, mashabiki wa Simba na Yanga walipoteza fahamu kulingana na hali ya jua kali na msalaba mwekundu walifanya kazi kubwa ya kutoa huduma ya kwanza.

Suala la usalama wa raia na mali zao lilikiwa vizuri baada ya Polisi kuwapo wengi uwanjani asubuhi na mapema kwa ajili ya kufanya majukumu yao ndani na nje ya uwanja.

Mashabiki wa timu zote mbili Simba na Yanga walijitokeza kwa wingi kuanzia saa moja asubuhi kwa lengo la kuwahi kuingia mapema uwanjani kulingana na maelekezo yaliyotolewa na mhusika wa usalama.

Mashabiki walikuwa wengi sana na ilipofika saa 6:00 tayari Simba na Yanga walifanikiwa kujaza majukwaa yote ya Sh. 15,000 na 10,000.

Ilikuwa ni kama Dar es Salaam yote imehamia Kigoma, baada ya mji huko kufurika kwa watu wa mpira wa miguu na wafanyabiashara wa mkoa huo kuona imeingia neema.

LWANGA MCHEZAJI BORA

Mfungaji wa bao la Simba, Taddeo Lwanga alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Imeandikwa na Somoe Ng'itu, Saada Akida na Adam Fungamwango.