Simba bingwa rasmi 2019/20

29Jun 2020
Somoe Ng'itu
Mbeya
Nipashe
Simba bingwa rasmi 2019/20
  • Yafikisha pointi 79 ambazo hazitafikishwa na timu nyingine, kukabidhiwa kikombe cha ubingwa mkoani Lindi kwa...

SIMBA imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Prisons katika mchezo wa ligi hiyo, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini hapa.

Wachezaji wa Simba wakiwapungia mikono mashabiki. PICHA: MAKTABA

Ubingwa huo ni watatu mfululizo baada ya kikosi hicho cha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck kufikisha pointi 79 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine, huku zikiwa zimebakia mechi sita msimu huu kumalizika huku Prisons wakifikisha pointi 43.

Nafasi ya pili katika msimamo wa ligi inashikiliwa na Yanga yenye pointi 60 na wakishinda mechi zote watafikisha pointi 78 wakati yenyewe itafikisha pointi 77.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa kila upande kutofanikiwa kuliona lango la mwenzake, lakini wenyeji wakionekana kutamba zaidi kwenye eneo la kiungo.

Mbali na kiungo kuonyesha uwezo wake, pia Salum Kimenya na Adili Buha walikuwa katika kiwango bora zaidi wakilisumbua lango la Simba mara kwa mara, lakini kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Aishi Manula alikuwa makini kuondoa hatari hizo.

Prisons inayonolewa na Mohammed Rishard 'Adolph' walianza kwa kasi katika mchezo huo na ilifanya shambulizi safi kupitia kwa mshambuliaji wake, Jeremiah Juma, lakini Manula aliwahi kusaka na kuwanyima Maafande hao bao la mapema dakika ya kwanza.

Wenyeji hao waliendelea kulisakama lango la Simba kwa kukaribia kufunga dakika ya 10 kupitia kwa Jeremia ambaye mpira wa kichwa aliyeunganisha kona iliyopigwa na Kimenya, kwa mara nyingine Manula akaudaka mpira huo.

Kipa wa Prisons, Jeremiah Kisubi aliinyima Simba bao baada ya kudaka kwa ufundi mpira wa faulo uliopigwa na Ibrahim Ajibu dakika ya 13 wakati krosi iliyopigwa na Kimenya ilikosea kipimo kidogo na kuwafanya Maafande hao kupoteza nafasi hiyo.

Dakika ya 30 Ezekia Mwashilindi alikaribia kuipatia Prisons bao, lakini Tanzania One Manula alipangua shuti hilo huku Kisubi naye alipangua mpira uliopigwa na Gerson Fraga na kuwabana Wekundu wa Msimbazi nafasi hiyo nyingine ya kufunga goli dakika ya 37.

Simba nayo ilianza kwa kasi kipindi cha pili kwa shambulio lililoanzia kwa Meddie Kagere, lakini pasi yake iliyokwenda kwa Miraji Athumani 'Sheva' ilitolewa nje na Kisubi dakika ya 47.

Manula aliwahi kupangua krosi safi iliyopigwa na Mwashilindi iliyokuwa inaelekea langoni moja kwa moja dakika ya 71 na shambulio lingine dakika iliyofuata kupitia kwa Samson Mbangula, lakini safari hii ukaishia mikononi mwa Manula.

Prisons walifanya shambulizi lingine sekunde chache baadaye, lakini Jeremiah alipiga shuti fyongo na kupoteza nafasi nyingine katika mchezo ambao uliohudhuriwa na Naibu Spika, Tulia Ackson.

Tanzania Prisons; kikosi kilikuwa na Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhilly, Salum Kimenya, Ezekia Mwashilindi, Samsom Mbangula, Jumanne Juma na Adily Buha.

Simba; Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Gerson Fraga, Hassan Dilunga/ Luis Miquissone (dk 67), Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/ Clatous Chama (dk 46) na Miraji Athumani 'Sheva'/ John Bocco (dk 80).

KOMBE KUKABIDHIWA LINDI

Taarifa za awali zilizopatikana jijini hapa zinasema, Simba itakabidhiwa kikombe cha ubingwa Julai 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa baada ya kumaliza mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Namungo FC.

Hata hivyo, Simba itakuwa na mchezo mwingine katika Kanda ya Kusini, Julai 5, mwaka huu dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Habari Kubwa