Simba haiwezekani tena

14Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe Jumapili
Simba haiwezekani tena
  • *Kiiza ‘Diego’ kinara wa mabao asiyepingika

SIMBA SC jana ilikwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2013 huku kocha wa muda Msimbazi, Jackson Mayanja, akitamba kuwa 'lazima wataifunga Yanga Jumamosi ijayo'.

WACHEZAJI WA SIMBA

Magoli mawili ya straika Hamis Kiiza yalimpa kocha huyo ushindi wa 2-1 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ikiwa ni mara ya sita mfululizo kikosi cha Simba chini ya Mganda huyo kinatoka kifua mbele Ligi Kuu.

"Nimefurahi kuona tumefanikisha lengo letu la kupata pointi sita hapa (Shinyanga)," Mayanja alisema. "Ushindi huu ni muhimu sana kwetu, unatupa nguvu ya kuikabili Yanga tukiwa na ari. Tunapaswa kushinda mechi ijayo. Na ni lazima tushinde dhidi ya Yanga ili iwe rahisi kwetu kutwaa ubingwa msimu huu."

Matokeo hayo yaliifanya Simba ikwee kileleni mwa msimamo wa VPL kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13 ikifikisha pointi 45 baada ya mechi 19, pointi mbili mbele ya Yanga wanaokamata nafasi ya pili.

Tangu msimu wa 2012/13 ambao Yanga walitwaa ubingwa licha ya kuanza vibaya kwa kutoka suluhu jijini Mbeya dhidi ya Prisons kabla ya kupoteza ugenini 3-0 na 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar, timu hiyo ya Msimbazi ilikuwa haijawahi kuonja raha ya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Azam FC, Mtibwa Sugar, Yanga na Ndanda FC ndizo timu pekee ambazo kwa nyakati tofauti ziliwahi kuongoza msimamo wa VPL katika misimu miwili iliyopita.

Simba itaendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa Azam FC watashindwa kuibuka na ushindi wa kuanzia magoli 3-1 watakapoikabili Coastal Union jijini Tanga leo jioni.

Dakika nne baada ya nusu saa ya mchezo, akiwa nje kidogo mwa boksi, mshambuliaji Hamis Kiiza alifungia Simba goli lililodumu kipindi chote cha kwanza akimalizia kwa shuti kali la mguu wa kulia kazi nzuri ya straika aliye katika kiwango cha juu, Ibrahim Ajibu aliyegongeana vyema na kiungo Mwinyi Kazimoto anayekabiliwa na tuhuma za kupiga mwandishi wa habari wa kike.

Lilikuwa bao la 15 kwa Mganda huyo lililomfanya aongoze chati ya wafumania nyavu hatari msimu huu akimuacha kwa goli moja Mfungaji Bora wa VPL 2013/14, Mrundi Amissi Tambwe wa Yanga.

Kama ilivyokuwa katika mechi ya Mwadui FC dhidi ya Simba mjini hapa Desemba 26 mwaka jana, mara tu baada ya kupulizwa kwa kipenga cha mwisho kipindi cha kwanza, kulinyesha mvua mjini hapa.

Mvua hiyo iliongezeka zaidi katika saa ya mchezo na kuonekana kuwa na faida kwa wenyeji ambao walizidisha mashambulizi langoni mwa Simba, lakini kipa wa kimataifa kutoka Ivory Coasta, Vincent Angban alikuwa mwiba kwao.

Kabla ya mvua hiyo kuongezeka na kuharibu ladha ya soka mjini hapa, Kiiza alitumia dakika mbili tu za kipindi cha pili kuandikisha goli la 16 kwake msimu huu na la pili kwa timu yake jana akimalizia kwa kichwa krosi murua iliyomiminwa ndani ya boksi la Stand United na beki wa pembeni kulia, Hassan Kessy.

Kiiza alipata nafasi nzuri ya kupiga 'hat-tick' ya pili msimu huu, lakini shuti lake la mguu wa kulia liligonga mwamba katika dakika ya 87.

Dakika mbili baadaye, straika 'kinda' Pastori Athanas aliwafuta machozi Stand United akitumia mwanya wa makosa ya beki Mrundi Emery Nimubona aliyerudisha mpira 'kizembe' kwa kipa Angban. Straika huyo aliunasa mpira huo na kuandikisha goli la pili Simba kufungwa tangu kocha Mayanja akabidhiwe mikoba ya Dylan Kerr aliyetimuliwa Januari 10.

Vikosi vilikuwa:

Stand United: Frank Muwonge, Revocatus Richard, Seleman Mrisho, Nassor Masoud, David Ossuman, Jacob Masawe, Pastory Athanas, Amri Kiemba, Seleman Selembe/ Jremiah Katura (dk 49), Seif Banda/ Elias Maguli (dk 49) na Vitalis Mayanga/ Fred Hamis (dk 75).

Simba: Vincent Angban, Hassan Kessy/ Mussa Mgosi (dk 86), Emery Nimubona, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/ Brain Majwega (dk 50), Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajibu/ Danny Lyanga (dk 66) na Said Ndemla.

Baada ya mchezo huo, Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ akasema timu itakwenda Uganda au Pemba kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu, Yanga SC Jumamosi ijayo – maana yake mpango wa kuweka kambi Morogoro unaweza kufa.

NDANDA 1-0 MAJIMAJI
Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, wenyeji Ndanda FC waliiibuka na ushindi wa pili mfululizo nyumbani wakiichapa Majimaji goli 1-0. Shukrani kwa Kigi Makasi aliyetupia katika dakika ya 75.
MATOKEO MENGINE
Mgambo JKT 0 - 1 African Sports
Mbeya City 5 - 1 Toto Africans
JKT Ruvu 1 - 1 Kagera Sugar
Imeandikwa na Sanula Athanas, Lasteck Alfred (Shinyanga) na Juma Mohamed (Mtwara)

Habari Kubwa