Simba hasira Azam kwa Mwadui FC

14Sep 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Simba hasira Azam kwa Mwadui FC

WAKATI ikielezwa kuwa benchi la ufundi la Simba limepewa mechi tano kujitathmini kama linastahili kuendelea kuinoa timu hiyo ama la, sare dhidi ya Azam, imepandisha mzuka kwa makocha wa timu hiyo na sasa limepanga kujisahaulisha matokeo hayo kwenye mchezo dhidi ya Mwadui ya Shinyanga hapo Jumapili.

Jackson Mayanja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kocha msaidizi wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa, Jackson Mayanja, alisema wanataka kurejea kwenye kasi waliyoanza nayo ligi kwa kupata ushindi mnono dhidi ya Mwadui FC.

Alisema sare waliyoipata dhidi ya Azam licha ya kuwahuzunisha mashabiki wao, pia iliwanyon'gonyesha wachezaji na benchi la ufundi.

"Kwa sasa tupo kwenye maandalizi dhidi ya Mwadui, tunataka kusahau matokeo yaliyopita, kama nilivyosema awali ligi ni ngumu si nyepesi, lakini kama Simba lazima turejee kwenye kasi yetu," alisema Mayanja.

Alisema wachezaji wake wanafahamu nini wanatakiwa kufanya na kwa sasa wanaendelea na mazoezi yanayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru ambao watautumia kwa mchezo huo.

NIYONZIMA HANA UHAKIKA
Kocha Mayanja, alisema hana uhakika kama kiungo wao fundi, Haruna Niyonzima, atauwahi mchezo huo wa Jumapili kutokana na malaria inayomsumbua tangu juzi.

Alisema kiungo huyo juzi na jana alishindwa kufanya mazoezi na wenzake kutokana na kusumbuliwa na malaria.

"Sina uhakika, japo mchezaji mwenyewe anatamani kuuwahi mchezo ujao, daktari anaendelea kufuatilia hali yake na tutaona itakavyokuwa," alisema Mayanja.

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi nne mbili nyuma ya Mtibwa Sugar iliyopo kileleni.

Wekundu wa Msimbazi hapo wanalingana pointi na watani zao Yanga, lakini ipo katika nafasi ya pili ikiwa na faida tofauti nzuri ya mabao kufunga na kufungwa.

Habari Kubwa