Simba: Hatujapata ofa ya Miquissone

28Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Hatujapata ofa ya Miquissone
  • ..Mangungu asema hakuna mchezaji atayeondoka, Try Again adai wao wanafanya biashara wako…

KLABU ya Simba imesema haijapata ofa toka kwenye klabu yoyote inayomhitaji mchezaji wake, Luis Miquissone raia wa Msumbiji

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kuwa hakuna mchezaji atakayeondoka mpaka pale watakapokaa na benchi la ufundi kuangalia ni vipi wakisuke tena kikosi chao cha msimu ujao kiwe tishio kuliko msimu huu, ndipo mengine yafuate.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', yeye amesema kuwa habari hizo ambazo zimeenea kila kona nchini na hata nje ya mipaka ya Tanzania, hazina ukweli kwa sababu hakuna klabu yoyote iliyokuja kwao kumtaka mchezaji huyo.

"Mezani hakuna kitu kama hicho. Hatujapata ofa yoyote ya klabu yoyote kumtaka mchezaji wetu Luis," alisema Try Again.
Hata hivyo, alisema iwapo kuna klabu yoyote inamhitaji wao wako tayari kumuuza kwa sababu pamoja na soka, lakini wanafanya biashara.

"Kama kuna timu inamhitaji ije tu. Sisi tunafanya biashara na hatumzuii mchezaji. Mwenye uwezo aje, hakuna tatizo," alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wake Mangungu alisema watalisikiliza benchi la ufundi kwanza baada ya mashindano kumalizika.

"Hatuwezi kusema lolote kwa sasa. Kwanza tutalisikiliza benchi la ufundi lituambie sehemu gani kuna mapungufu, nani atoke, nani abaki, nani aingie, ndipo tunapoweza sasa kutoka na kuzungumza nini kimefanyika," alisema.

Klabu mbalimbali zilizocheza Ligi ya Mabingwa Afrika zinatajwa kumwania mchezaji huyo machachari zikiwamo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri.

Hata hivyo, tetesi zinaitaja klabu ya Al Ahly ndiyo imeonekana kumhitaji zaidi kutokana na uwepo kwa kocha, Pitso Mosimane ambaye ameshawahi kumfundisha mchezaji huyo akiwa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Viongozi hao wa Simba kila mmoja alisema kuwa baada ya msimu wao kumalizika ukiwa wa mafanikio, wanatarajia kukisuka tena kikosi chao kwenye baadhi ya maeneo ili kuendelee kuwa cha kutisha barani Afrika, achilia mbali Ligi Kuu ya Tanzania kwa msimu ujao.