SIMBA HESHIMA MWANZO MWISHO

10Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
SIMBA HESHIMA MWANZO MWISHO

KLABU ya Simba sasa inatembea kifua mbele kutokana na kujiridhisha kuwa na kikosi kizuri kuelekea msimu ujao, hiyo ikiwa ni baada kuifunga mabao 4-0 timu ngumu, AFC Leopard ya Kenya katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Simba ilisherehekea vyema kutimiza miaka 80 Jumatatu kwa kucheza mchezo wa kirafiki na AFC Leopard na kuibuka na ushindi huo ambao umeleta faraja kwa timu hiyo kuelekea kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 20, mwaka huu.

Akizungumza na Lete Raha jana, Kocha Mkuu wa Simba, Omog, alisema amevutiwa na wachezaji kwa ujumla baada ya mechi ya Jumatatu na amewaagiza viongozi waandae mchezo mwingine wa kirafiki mapema iwezekanavyo.

“Nimefurahi timu yangu ilivyocheza. Wachezaji wamenifurahisha kwa ujumla, sasa ninakwenda kufanyia kazi upungufu uliyojitokea, kabla ya mchezo mwingine, nadhani tutacheza na timu ya Uganda,”alisema.

Mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Ajibu, aliendelea kumvutia kocha mpya, Mcameroon Joseph Omog baada ya kufunga mabao mawili, huku wachezaji wapya, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga pia bao moja kila mmoja.

Kadhalika, wachezaji wote wapya waliopangwa mbali ya Kichuya na Mavugo, walicheza vizuri. Hao ni Janvier Bokungu, Hamad Juma, Method Mwanjali, Jamal Mnyate, Mussa Ndusha, Muzamil Yassin, Frederick Blagnon na Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji ya Simba SC chini ya Rais wake, Evans Aveva, inatarajiwa kukutana na mfanyabiashara Mohamed ‘MO' Dewji’ Jumatatu ya wiki ijayo mjini Dar es Salaam.

Katibu wa Simba SC, Patrick Kahemele, amelimbia Lete Raha kuwa wameshamtumia taarifa MO juu ya kikao hicho cha wiki ijayo.

Bilionea huyo namba 21 Afrika, amewasilisha barua kutaka kununua asilimia 51 ya hisa za Klabu ya Simba kwa Sh. bilioni 20.