Simba imeitendea haki Visit Tanzania

25Feb 2021
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba imeitendea haki Visit Tanzania

WAZIRI wa Utalii na Maliasili, Dk. Damas Ndumaro, amesema Simba imeitendea haki kwa kiwango cha juu jezi yao yenye ujumbe wa 'Visit Tanzania' katika mechi zake za hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliingia makubaliano na serikali kwa kuvaa jezi yenye ujumbe huo kwenye mechi zake baada ya mdhamini wake Sportpesa kukinzana na mdhamini mwingine wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Ndumbaro ametoa kauli hiyo baada ya Simba kupata ushindi mara mbili mfululizo, ugenini dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na Al Ahly iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi hao wa Tanzania maarufu Wekundu wa Msimbazi walipata ushindi wa bao 1-0 Mjini Kinshasa, DRC juzi wakapata tena ushindi kama huo dhidi ya vigogo wa Afrika kutoka Misri.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ndumbaro alisema wataendelea kushirikiana na Simba kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo yanaendelea barani Afrika.

Waziri huyo alisema pia watahakikisha michezo yote inafanya vyema katika mashindano ya kimataifa na kuendelea kutangaza jina la Tanzania vizuri.

"Tunaipongeza sana Simba kwa kazi nzuri waliyofanya, kiukweli wameitendea haki zaidi Visit Tanzania katika mechi zote mbili walizocheza, tutahakikisha wanaendelea kufanya vizuri kwenye michezo inayofuata, na hii haitaishia kwa Simba tu, tunataka kuona michezo yote inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa," Ndumbaro alisema.

Simba yenye pointi sita ndio inaongoza katika msimamo wa Kundi A ikifuatiwa na Al Ahly yenye pointi tatu sawa na AS Vita huku Al Merrikh ambayo imepoteza mechi zake mbili ilizocheza ikiburuza mkia kwenye kundi hilo.

Baada ya mechi hiyo ya juzi, Simba sasa itasafiri kuelekea Khartoum, Sudan kuwafuata Al Merrikh kati ya Machi 5 na 6, mwaka huu halafu itarejea nyumbani kuwasubiri Wasudani hao.

Mechi itakayofuata itachezwa mapema Aprili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya AS Vita na itamalizia hatua ya makundi nchini Misri dhidi ya Al Ahly.

Habari Kubwa