Simba inang'ata tu Yanga yazinduka

08Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
Simba inang'ata tu Yanga yazinduka
  • *Ajibu alikosa penalti huku Barthez akipangwa kwenye kikosi cha Yanga kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 28 walipotoka sare ya 2-2 dhidi ya Mwadui FC mjini Shinyanga.

MOTO wa Simba umeendelea kuitikisa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya jana kuibuka na ushindi wa bao1-0 dhidi ya Kagera Sugar iliyobaki na wachezaji 10 uwanjani mjini Shinyanga huku Yanga wakizinduka kwa kuichapa JKT Ruvu magoli 4-0 jijini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yaliwafanya Yanga waendelee kukaa kileleni mwa msimamo wa VPL wakiwa na mtaji wa pointi 43, moja nyuma ya Simba wanaokamata nafasi ya pili, lakini wakiwa na pointi sawa na Azam FC ambao jana pia walishinda goli 1-0 dhidi ya Mwadui FC.
Baada ya kushinda mechi zote mbili tangu wahamie kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Kagera Sugar walishindwa kukizuia kikosi cha kocha mkuu wa muda Jackson Mayanja walipokubali kipigo cha bao 1-0 na kuipa Simba ushindi wa tano mfululizo chini ya Mganda huyo.
Goli pekee la mechi hiyo ya raundi ya 18, lilifungwa na mshambuliaji Ibrahim Ajibu aliyemalizia kwa shuti la mguu wa kulia pasi ya kisigino aliyopewa na ndani ya boksi na kinara wa mabao Hamis Kiiza ambaye alipokea krosi nzuri ya kiungo mzoefu Mwinyi Kazimoto.
Ajibu alipata nafasi ya kufunga goli lake la tisa msimu huu, lakini penalti yake ya shuti 'mtoto' la mguu wa kulia ilipanguliwa na kipa Andrew Mtara. Penalti hiyo ya tatu Simba kupewa msimu huu, ilitolewa na refa Mathew Akrama wa Mwanza baada ya Juma Jabu kumvuta bega straika huyo wa Msimbazi.
Kikosi cha kocha Adolf Richard kililazimika kumalizia dakika za mwisho kikiwa pungufu baada ya Daudi Jumanne kulimwa kadi nyekundu na refa Akrama, jambo ambalo lilionekana kuwakera wenyeji ambao baada ya kipenga cha mwisho, walimvaa mwamuzi huyo kabla polisi kumnusuru.

Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, baada ya kufunga kwa tuta mjini Mbeya Jumatano na kuinusuru timu yake kulala dhidi ya Prisons, nyota ya Simon Msuva iliendelea baada ya jana kutupia mara mbili wakati Yanga ilipozinduka na kushinda 4-0 dhidi ya timu 'kibonde' ya JKT Ruvu.
Mchezaji Bora huyo wa VPL msimu uliopita, alitumia dakika 12 kuandika goli la kwanza la mabingwa watetezi akifumua shuti la upinde wa mvua kwa mguu wa kushoto akiwa m 18 kutoka lango la kaskazini mwa uwanja huo baada ya kurushiwa mpira na beki wa pembeni kulia, Juma Abdul.
Winga wa usajili wa dirisha dogo, Isoufou Boubacar, aliihakikisha Yanga kupumzika ikiwa mbele kwa magoli 2-0 akifumua shuti kali la mguu wa kushoto ndani boksi dakika tatu kabla ya robo tatu ya saa ya mchezo.
Lilikuwa goli la kwanza kwa Mnigeria huyo kuifungia Yanga VPL na la pili kwake katika mashindano yote msimu huu baada ya kufunga pia katika ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mechi yao ya hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mwezi uliopita.
Mshambuliaji anayeibeba Yanga msimu huu, Donald Ngoma alifunga goli lake la 10 na la tatu kwa timu yake jana akimalizia kwa kichwa krosi ya Abdul iliyotua ndani ya boski dakika tatu baada ya saa ya mchezo.
Msuva alitupia la nne dakika ya 90+3 akitendea haki kazi nzuri iliyofanywa na mshambuliaji wa usajili wa dirisha dogo msimu huu, Paul Nonga ambaye alitokea benchini.

AZAM 1-0 MWADUI
Kwenye viunga vya Azam Complex, kikosi cha kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' cha Mwadui FC kilishindwa kusahihisha makosa yaliyokigharimu katika kipigo cha bao 1-0 dhidi ya African Sports Jumatano baada ya jana kufungwa tena 1-0 na Azam FC jijini Dar es Salaam.
Straika wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche, alifunga goli lake la saba msimu huu akimalizia kwa shuti la mguu wa kulia kazi nzuri iliyotokana na gonga ya pasi sita nje katika dakika ya 19 ya mechi yao.
Mwadui pia ilifungwa bao 1-0 na Wanalambalamba katika mechi yao ya kwanza msimu huu kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga.

NDANDA 1-1 MTIBWA
Mjini Mtwara, wenyeji Ndanda FC walilazimika kusubiri hadi dakika ya 84 kusawazisha goli la dakika ya 30 la Mtibwa Sugar lililofungwa na Seleman Rajabu aliyemalizia mpira wa kona ya Isa Rashid 'Baba Ubaya' iliyotemwa na kipa Jeremia Kisubi.
Bryson Raphael, anayekipiga Ndanda FC kwa mkopo kutoka Azam FC, ndiye aliyeokoa jahazi kwenye Uwanja wa Nangwanda akifunga katika mechi mbili mfululizo baada ya kutupia pia goli pekee la mechi yao iliyopita ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union.

MAJIMAJI 1-0 MGAMBO
Majimaji FC ambayo Jumatano ililala 2-1 dhidi ya Kagera Sugar mjini Shinyanga, ilizinduka na kuichapa Mgambo JKT bao 1-0 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Shukrani kwa goli pekee la Danny Mrwanda aliyetupia katika dakika ya 23. Mchezaji huyo wa zamani wa Simba, alifunga pia katika kipigo cha 2-1 dhidi ya Kagera Sugar.

TOTO 2-0 COASTAL
Coastal Union inaonekana 'kulewa' na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga baada ya jana kukubali kichapo cha pili mfululizo ilipofungwa 2-0 dhidi ya Toto Africans mjini Mwanza. Coastal pia ilifungwa 1-0 dhidi ya Ndanda FC Jumatano

Mbeya City 0-0 Prisons
Benjamini Asukile wa Tanzania Prisons alilimwa kadi nyekundu katika dakika ya mwisho ya mechi ya watani wa jadi wa jiji la Mbeya baada ya kumkanyaga Ramadhani Chombo 'Redondo'.

Imeandikwa na Lasteck Alfred (Shinyanga), Nebart Msokwa (Mbeya), Juma Mohamed (Mtwara), Somoe Ng'itu na Sanula Athanas (Dar).

Habari Kubwa