Simba kazi moja nusu fainali FA

14May 2022
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba kazi moja nusu fainali FA

IWAPO Simba itashinda leo kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Pamba, itakutana na watani wake wa jadi Yanga kwenye mechi ya nusu fainali, kusaka bingwa atakayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka barani Afrika.

Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Simba itakuwa na kazi moja tu kupata ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea tena kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema maandalizi yamekamilika na kinachosubiriwa ni kuingiza timu uwanjani.

"Tumejiandaa na mchezo huu mgumu, kucheza na timu ambayo haina cha kupoteza ni hatari kubwa. Pamba kufika hatua ya robo fainali kwake ni mafanikio makubwa, ukicheza na timu iliyoridhika ni hatari sana, tutaingia kwa tahadhari na kwa kuiheshimu kwa sababu mpira una maajabu yake na Simba tumeshawahi kupitia maajabu hayo," alisema Ahmed.

Simba ilishawahi kutolewa kwenye kombe hilo kwa nyakati tofauti dhidi ya timu za Mashujaa FC ya Kigoma na Green Warriors ya Dar es Salaam.

"Lakini kwa sisi Simba ni jukumu letu kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mechi hii kwa kuishikisha adabu Pamba ili tuweze kuingia hatua ya nusu fainali, hakuna mtu atakayetuelewa duniani hapa kama tukitolewa na Pamba," alisema Ahmed.

Katibu Mkuu wa Pamba, Johnson James amekiri mechi itakuwa ngumu kutokana na ubora ambao Simba imekuwa ikiuonesha kwenye mechi za hivi karibuni, lakini hawaiogopi.

"Hatuwezi kuiogopa Simba kwa sababu tumeingia hapa kwa uwezo wetu, hata kufika hatua hii tumeifunga Dodoma Jiji, timu ya Ligi Kuu kama ilivyo Simba. Hatukupata nafasi hii kwa bahati mbaya tuna timu bora, mwanzo kilichotusumbua ni hali ya hewa, lakini kwa sasa tumekaa wiki nzima hapa tangu tucheze mechi ya Championship, kwa hiyo haitotusumbua tena," alisema Katibu Mkuu huyo.

Pamba ipo Dar es Salaam tangu Mei 8, ilipocheza mechi ya Championship dhidi ya DTB na kufungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, mechi ambayo iliwapandisha Ligi Kuu wapinzani wao hao.

Simba itakuwa inasaka nafasi ya kucheza nusu fainali dhidi ya Yanga, msimu uliopita ilicheza fainali kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma Julai 25, 2021 na kushinda bao 1-0.

Na iwapo kama zitakutana nusu fainali itakuwa ni mara ya kwanza tangu Julai 12, 2020 zilipokutana kwenye hatua hiyo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikishinda mabao 4-1.

Yanga ambayo inamsubiri mshindi kati ya Simba au Pamba, iliingia hatua hiyo kwa kuitwanga Geita Gold kwa mikwaju ya penalti 7-6, baada ya sare ya bao 1-1.

Habari Kubwa