Simba, Kichuya raha utamu

16Oct 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba, Kichuya raha utamu
  • *** Yang'ara Kichuya akikaa kileleni kwa kamba saba, Stand nayo haifungiki baada ya...

MUZAMIL Yassin aliifungia Simba bao la kuongoza katika dakika ya 43, wakati wakishinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar jana, lakini raha na utamu wa mechi hiyo kwa mashabiki wa timu hiyo ililipuka baada ya Shiza Kichuya kuziona nyavu kipindi cha pili.

Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, akishangia baada ya kufunga kwa mkwaju wa Penalti katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru jana. Simba ilishinda 2-0. PICHA: MICHAEL MATEMANGA

Kila kona ya Uwanja wa Uhuru jana mashabiki walikuwa wakilitaja jina la Kichuya ambaye hilo ni bao lake la saba tangu kuanza msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kichuya aliyefunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 75 baada ya mwamuzi Hussein Athumani kutoka Katavi kuyaona madhambi ya Mohd Ibrahim aliyemwangusha Juma Ramadhani ndani ya boksi, ndiye anayeongoza kwa ufungaji katika ligi hiyo.

Omary Mponda wa Ndanda anashika nafasi ya pili kwa ufungaji akiwa na mabao matano huku Amissi Tambwe (Yanga) akiwa na manne.

Muzamil ambaye amejiunga na Simba akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, hilo ni bao lake la kwanza kwake na alilitia nyavuni akiunganisha kona iliyochongwa na Kichuya.

Hata hivyo, Simba inayofundishwa na Mcameroon Joseph Omog, ilionyesha kuwa na njaa ya mabao lakini mshambuliaji wake kutoka Ivory Coast Fredrick Blagnon alishindwa kutumia nafasi mbalimbali licha ya kutengewa krosi na pasi za mabao.

Dakika ya nne beki wa Kagera Sugar Mwaita Gereza aliwahi kuokoa mpira na kuutoa nje na kumfanya Blagnon ashindwe kufunga bao ndani ya 18.

Ibrahim Ajibu alipiga shuti fyongo na kupoteza krosi ya Mwinyi Kazimoto na kushindwa kuipatia timu yake bao katika dakika ya 14.

Kagera Sugar ilijibu shambulio hilo, lakini Godfrey Taita aliyepokea krosi ya Selemani Mangoma alipaisha juu na kupoteza nafasi hiyo ya kufunga huku mabeki wa Simba wakiwa wamekatika kwenye eneo lao la ulinzi dakika ya 17 ya mchezo huo.

Simba ilipoteza tena nafasi ya kufunga baada ya kipa wa Kagera Sugar, Mohamed Shariff 'Casillas' kudaka mpira uliopigwa kwa kichwa na Blagnon aliyepokea pasi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Simba: Vincent Angbam, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Murshid Juuko, Method Mwanjali, Shiza Kichuya, Mzamilu Yassin, Jonas Mkude, Fredrick Blagnon/ Mavugo (dk.56), Ibrahim Ajibu/Mohd Ibrahim (dk.60) na Mwinyi Kazimoto.

Kagera Sugar: Mohammed Hussein 'Casillas', Mwaita Gereza, Godfrey Taita, Juma Ramadhani, George Kavila, Selemani Mangoma, Ally Nassor, Shabani Sunza, Danny Mrwanda/Themi Felix (dk.62) , Christopher Edward/ Paul Ngwai (dk.52) na Mbaraka Abeid.

Stand haifungiki
JKT Ruvu ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya bao1-1 na Mwadui FC, wakati katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Stand United iliendelea kulinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo msimu huu baada ya kutoka sare 1-1 dhidi African Lyon.

Habari Kubwa