Simba kufunga hebabu kibabe

08Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kufunga hebabu kibabe

WAKATI wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, wakiwasili salama jijini Cairo, beki wa timu hiyo, Mkenya Joash Onyango, amesema wamekwenda nchini Misri kwa lengo la kupambana kusaka ushindi dhidi ya wenyeji Al Ahly na si kukamilisha ratiba.

Al Ahly inatarajia kuwakaribisha Simba katika mechi ya mwisho ya Kundi A itakayochezwa kesho huku timu hizo mbili tayari zikiwa zimefuzu kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Akizungumza na gazeti hili kabla ya kuondoka nchini juzi, Onyango alisema licha ya timu yao kufuzu hatua inayofuata, hawatabweteka katika mchezo huo wa mwisho dhidi ya vigogo hao wa Afrika.

Onyango alisema ubora unaoonyeshwa na kikosi chao unatokana na malengo waliyojiwekea pamoja na umoja waliokuwa nao ndani ya timu hiyo ambayo pia inashikilia taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Tumefuzu hatua ya makundi lakini hiyo pekee haitufanyi tuingie katika mchezo dhidi ya Al Ahly tukiwa tumeridhika,
tunahitaji kutafuta matokeo mazuri, tutapambana kwa ajili kutimiza malengo yetu ya msimu huu,” alisema Onyango.

Beki huyo aliongeza wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo huo na watahakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yao ili kupata matokeo chanya katika mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 4:00 usiku.

"Hautakuwa mchezo rahisi, tutacheza kwa tahadhari na nidhamu ya hali ya juu, kwa sababu Al Ahly ni timu nzuri, inahitaji kufanya vizuri nyumbani kwao, hata sisi tumejipanga kutafuta matokeo mazuri ugenini,"alisema Onyango.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa hapa nchini, Simba ambao ni vinara wa Kundi A wakiwa na pointi 13 mkononi walipata ushindi wa bao 1-0, mfungaji akiwa ni Luis Miquissone.

Habari Kubwa