Simba kuikabidhi Yanga ubingwa leo?

08May 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba kuikabidhi Yanga ubingwa leo?

SIMBA inaingia kwenye kibarua kigumu leo itakapomenyana na Mwadui FC kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kwenye uwanja wa Taifa lakini matokeo yoyote zaidi ya ushindi yatakuwa yamirasimisha Yanga kutwaa ubingwa msimu huu.

Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 58 baada ya Shirikisho la soka nchini (TFF) kuipokonya pointi tatu Azam FC iliyokuwa nafasi ya pili kwa pointi 59 (sasa ina pointi 56) imepisha na Yanga kwa pointi 10 ingawa Yanga wana mchezo mmoja zaidi ya Simba.

Endapo Simba itapoteza mchezo wa leo kutatoa fulsa kwa Yanga kujitanga mabingwa kabla awajamaliza michezo yao mitatu iliyobakia.

Hiyo inamaana kwamba Simba akifungwa leo hatokuwa na uwezo tena wa kuzifikia pointi 68 za yanga hata kama watashinda kwenye michezo yao yote iliyobakia na YAnga kuupoteza michezo yao.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha wa Simba, Jackson Mayanja, alisema kuwa hawatakuwa tayari kuona Yanga wakitangaza ubingwa kwa mgongo wa Simba hivyo watahakikisha wanashinda mchezo wa leo.

"Kimahesabu ni ngumu sana kwetu kutwaa ubingwa, lakini kwenye mpira lolote linaweza kutokea, tutapambana mpaka mchezo wetu wa mwisho na tutahakikisha tunashinda," alisema Mayanja.

Alisema kuwa mchezo wa leo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao lakin i watapambana na kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki.

Kwa upande wake, Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri kiwhelo 'Julio' alisema kuwa watashuka kwenye uwanja wa Taifa kwa ajili ya kusaka ushindi.

"Tumejiandaa vizuri, najua udhaifu wa Simba hivyo tutaingia uwanjani kwa lengo la ushindi tu, na siku zote ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni," alisema Kiwhelo.

Endapo Simba itaibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo, utaichelewesha Yanga angalau kwa wiki moja kabla haijatangaza ubingwa.

Kikosi hicho cha Kocha Hans van der Pluijm, kinaitaji pointi nne pekee kutangaza ubingwa.

Habari Kubwa