Simba kuing'oa tena Yanga kileleni leo?

10Mar 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Simba kuing'oa tena Yanga kileleni leo?
  • Timu hiyo ya Msimbazi itaikabili Ndanda FC jijini Dar es Salaam wakati City na Stand zikionyeshana kazi Mbeya.

SIMBA itahitaji ushindi kuishusha Yanga kileleni wakati itakapoikabili Ndanda FC katika mechi ya raundi ya 22 ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo jioni.

Kikosi cha Simba.

Timu hiyo Msimbazi kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa pointi mbili nyuma ya Wanajangwani wenye pointi 50 baada ya mechi 21.

Yanga walishinda 5-0 dhidi ya African Sports juzi na kurejea tena kileleni mwa ligi hiyo wakiwang'oa watani wao wa jadi walioongoza kwa saa 48 waliposhinda 2-0 dhidi ya Mbeya City FC Jumapili.

Kikosi cha Simba kina nafasi kubwa ya kushinda mechi ya leo kutokana na rekodi nzuri kiliyonayo dhidi ya Ndanda. Timu hiyo ya Mtwara haijawahi kufunga goli hata moja dhidi ya Simba tangu ianze kushiriki Ligi Kuu msimu wa 2014/15, achilia mbali kushinda mechi.

Mabingwa mara 18 wa Tanzania Bara walishinda 2-0 mjini Mtwara kabla ya kuibamiza timu hiyo ya Masasi mabao 3-0 Dar es Salaam duru la pili msimu wa 2014/15 kisha wakatoka kifua mbele kwenye Uwanja wa Nangwanda kwa bao pekee la mechi lililofungwa na Ibrahim Ajibu siku ya kwanza ya mwaka huu.

Simba pia wanajivunia safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Mganda Hamisi Kiiza na mzawa Ibrahim Ajibu ambao kwa pamoja wametupia mara 24 kati ya 37 ya timu yao Ligi Kuu msimu huu.

Ukiviondoa vipigo viwili vya 2-0 dhidi ya Yanga na sare ya 2-2 dhidi ya Azam FC, Simba imeshinda mechi zingine zote ilizocheza kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu, jambo ambalo linaweza kuwa habari mbaya kwa Ndanda walioruhusu kufungwa magoli 20 (11 ugenini) na kufunga 19 katika mechi 21 zilizopita.

Kati ya mechi zote 10 walizocheza ugenini msimu huu, Ndanda ambao pia hawajawahi kufunga goli kwenye Uwanja wa Taifa, wameshinda moja (1-0 dhidi ya Coastal Union), sare nne na kupoteza tano.

BOBAN KUIKOSA STAND LEO
Katika mechi ngingine ya ligi ya Bara leo, kiungo Haruma Moshi 'Boban' hatakuwa sehemu ya kikosi cha Mbeya City FC kitakachoivaa Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kiungo huyo mzoefu anatarajiwa kurejea uwanjani Machi 14 baada ya Mkuu wa Kitengo cha Utabibu cha Citu, Dk. Joshua Kaseko kubainisha kuwa anasumbuliwa na Malaria.

“Ni wazi hatakuwa sehemua ya mchezo kesho (leo), ana Malaria tumeshamtaarifu mwalimu (Kinnah Phiri) juu. Atarejea kikosini MachI 14 wakati tutakapokuwa tunacheza dhidi ya Africans Sports jijini Tanga," alisema tabibu huyo jana.

City pia itakosa huduma ya Kenny Ally katika mechi ya leo kutokana na kiungo huyo kuwa na kadi tatu za njano pamoja na beki Deo Julius anayesumbuliwa na majeraha ya goti.

Mechi ya leo ni ya nne kwa timu hizo kukutana Ligi Kuu, Stand ikishinda mara mbili, huku City ikishinda mechi moja.

NDANDA FC UGENINI MSIMU HUU
1. Toto Africans 0 - 0 Ndanda FC
2. Coastal Union 0 - 1 Ndanda FC
3. Mgambo JKT 1 - 1 Ndanda FC
4. Yanga 1 - 0 Ndanda FC
5. Mwadui FC 2 - 1 Ndanda FC
6. Kagera Sugar 1 - 1 Ndanda FC
7. Prisons 2 - 2 Ndanda FC
8. Majimaji 1 - 1 Ndanda FC
9. African Sports 1 - 0 Ndanda FC
10. Mtibwa Sugar 2 - 1 Ndanda FC
----------------------------------

Habari Kubwa