Simba kuishukia Ruvu kama Vita

19Mar 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kuishukia Ruvu kama Vita
  • ***Yasema hakuna atayebaki salama Ligi Kuu, Magori afuata droo Caf robo fainali Misri huku...

TUMEREJEA! Baada ya kumaliza mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha Simba kimerejea kuendelea kusaka pointi tatu kwa kuwavaa Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam huku ikieleza ....

kuwa moto uliowalipua AS Vita ndio watakaoendelea nao.

Awali mechi hiyo ilitarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro lakini kutokana na baadhi ya wachezaji wa Simba kubanwa na kambi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) na wengine wa nje kutakiwa kusafiri leo usiku, mchezo huo umelazimika kurejeshwa Uwanja Taifa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema timu yake itaingia kwa kasi ile ile ya kusaka pointi tatu kama ilivyocheza katika mechi za mashindano ya kimataifa kwa sababu malengo yao ni kutetea taji hilo wanalolishikilia.

Rweyemamu alisema kuwa wachezaji wote ni wazima na jana asubuhi walifanya mazoezi isipokuwa nyota wake walioitwa katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kinajiandaa kuikaribisha Uganda (Cranes) Jumapili.

"Vijana wako vizuri na tunamshukuru Mungu Jumamosi hatukupata majeruhi, wamefanya mazoezi leo (jana) asubuhi na kwa kifupi tuko tayari kwa mechi hiyo ya kesho (leo) ambayo itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku," alisema Rweyemamu.

Aliongeza kuwa kila mchezo ulioko mbele yao ni sawa na fainali na wanahitaji "kuwakimbiza" Yanga na Azam ambao wanapointi nyingi zaidi na wamejiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni.

Naye kiungo wa kimataifa wa Simba Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliliambia gazeti hili kuwa wamejipanga kuendelea kuwapa furaha mashabiki wa timu yao baada ya Jumamosi iliyopita kuweka historia kwa kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Sio mimi tu, kila mchezaji wa Simba huwa yuko tayari kuisaidia timu na kufanya kile ambacho mwalimu ameelekeza, tunahitaji kushinda pia mechi zetu za Ligi Kuu ili kujihakikisha ubingwa kwa msimu wa pili, na kupata tena nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani," alisema kiungo huyo ambaye katika mechi dhidi ya AS Vita alionyesha kiwango cha juu.

Katika hatua nyingine, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alitarajiwa kuondoka leo kuelekea jijini Cairo, Misri tayari kushuhudia droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezeswa kesho.

Kwa upande wa Ligi Kuu, Yanga ndio wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 67, lakini wamecheza mechi 28 wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 59 baada ya mechi 28 na Simba yenye pointi 51 ni ya tatu kufuatia kushuka dimbani mara 20.

Ruvu Shooting ambayo imecheza mechi 30, ina pointi 35 na iko katika nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi wakati African Lyon iliyocheza michezo 31 ina pointi 22 na inaburuza mkia.

Habari Kubwa