Simba kuivaa Coastal bila Kiiza

11Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Simba kuivaa Coastal bila Kiiza

WEKUNDU wa Msimbazi leo wanatarajia kuikaribisha Coastal Union katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bila ya straika wake Hamisi Kiiza kutokana na kutimuliwa kambini juzi.

kikosi cha simba.

Kiiza aliamuriwa aondoke kambini Ndege Beach baada ya kukaidi agizo la kuvaa sare na kutumia basi la timu kwenda Uwanja wa Taifa kutazama mechi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya Yanga dhidi ya Al Ahly iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Simba iliyoko chini ya Mganda Jackson Mayanja msimu huu imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya mabingwa hao wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara mwaka 1988 baada ya kuwafunga nyumbani na ugenini na kuchukua pointi zote sita.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Machi 19 kwenye Uwanja wa Mkwakwani na kupitia washambuliaji Kiiza na Danny Lyanga, Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0 na kuwa timu pekee ya jijini Dar es Salaam iliyovuna pointi tisa kwenye uwanja huo.

Mayanja aliliambia gazeti hili juzi kwamba wamejiandaa vizuri kuivaa Coastal Union na hatimaye kusonga mbele kwenye michuano hiyo ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho mwakani.

"Timu yangu imejiandaa vizuri na mechi hiyo ya robo fainali, lengo letu ni kushinda na kusonga mbele, hatutaidharau Coastal Union kwa sababu haifanyi vizuri kwenye ligi," alisema Mayanja juzi alipozungumza na gazeti hili.

Yanga, Azam FC na Mwadui FC ya mkoani Shinyanga tayari zimeshafuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo yaliyorejea msimu huu.

Habari Kubwa