Simba kumaliza hasira kwa Ruvu

25Oct 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba kumaliza hasira kwa Ruvu

BAADA ya kupata kichapo katika mchezo uliopita, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamesema watamaliza 'hasira' za kufungwa watakapowakaribisha Ruvu Shooting hapo kesho kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kikosi chao kilianza mazoezi jana na kila mchezaji ameahidi kujirekebisha kuelekea mchezo huyo wa raundi ya nane.

Rweyemamu alisema wanafahamu kila mechi ya ligi ni muhimu, hivyo wataongeza umakini katika mechi ya leo kwa sababu malengo yao ni kutetea taji hilo wanalolishikilia.

"Ukimaliza mechi unafunga hesabu, huwezi kubadilisha matokeo, unaanza ukurasa mpya, sasa hivi kiufundi tunaiangalia Ruvu Shooting, ndio mtihani ulioko mbele yetu, tumeshaanza kuipigia hesabu, tujue tutamalizana nao vipi," alisema Rweyemamu.

Meneja huyo alisema wachezaji waliokuwa majeruhi wanaendelea vyema na kila mmoja anafanya mazoezi kulingana na programu aliyopewa na daktari.

"Watarudi, siwezi kusema lini, lakini kuna matumaini ya mapema, hakuna mwenye tatizo kubwa hadi sasa, mashabiki watawaona hivi karibuni," Rweyemamu aliongeza.

Mabingwa hao watetezi wana pointi 13, wameshinda mechi nne, wametoka sare mara moja na wamepoteza mchezo mmoja dhidi ya Tanzania Prisons Alhamisi iliyopita wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga, Rukwa.

Habari Kubwa