Simba kumruhusu Mkude kuondoka

09Dec 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kumruhusu Mkude kuondoka

MAKAMU wa Rais wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', amesema klabu hiyo ipo tayari kumruhusu kiungo wake Jonas Mkude kuondoka endapo atapata timu nje ya nchi.

Kaburu, alisema kuwa nahodha huyo wa Simba amebakisha mkataba wa zaidi ya miezi sita na kwa sasa haruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote kutokana na mkataba huo, lakini wanatambua ndoto za nyota huyo kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

"Mkude ni mchezaji wa Simba, na yeye anatambua hilo, tumefanya naye mazungumzo na amebainisha yeye ni Simba damu kwa sababu amelelewa na klabu hii hivyo kama ataamua kuendelea kucheza soka hapa nchini ataichezea Simba," alisema Kaburu.

Alisema kuwa mchezaji huyo kwa sasa bado yupo Simba na ataichezea timu hiyo kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu itakayoanza Desemba 17.

Kaburu aliweka wazi ujio wa kiungo mkabaji raia wa Ghana James Kotei sio kwa ajili ya kuziba pengo la Mkude kama inavyosemwa na baadhi ya wadau wa soka.

"Kuna makombe matatu mbele yetu, Kombe la Shirikisho, ligi kuu na kombe la Mapinduzi na haya yote tumepania kuyachukua sasa lazima tuongeze wigo wa wachezaji hatuwezi kuwa na mchezaji mmoja katika namba moja ni kumchosha ," alisema Kaburu.

Alisema usajili wanaoufanya umetokana na maombi ya kocha Joseph Omog aliyeomba kuongeza wachezaji kwenye nafasi ya golikipa na kiungo mkabaji.

Habari Kubwa