Simba kunuka noti, Sven aonya

14Jul 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kunuka noti, Sven aonya

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck amewataka wachezaji wake kutoridhika na kutwaa ubingwa pamoja na kuifunga Yanga na badala yake waelekeza akili na nguvu zao kwenye mechi zao zilizobaki ili kumaliza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa heshima kubwa.

Simba imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka nchini (FA Cup) kwa kuifunga Yanga mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Akizungumza na gazeti hili jana baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Sven alisema anawapongeza wachezaji wake kucheza vizuri na kufanikiwa kulipa kisasi kwa kuibuka na ushindi mkubwa katika mchezo huo, lakini akiwataka kutazama zaidi mechi zilizosalia.

Alisema nusu fainali ilikuwa nzuri kwa wapinzani wake kucheza vizuri kipindi cha kwanza pamoja na walivyopata bao la kwanza hali iliyompa wakati mgumu kuhawahimiza wachezaji wake kujitolea.

“Wamejituma wamecheza kwa kiwango kizuri, lakini bado hatujamaliza ligi, tunahitaji kufanya vizuri na kuheshimu ubingwa wetu kwa kutafuta alama muhimu katika mechi zetu za ligi ikiwamo dhidi ya Mbao FC,” alisema Sven.

Alisema kwa matokeo hayo pamoja na kutangazwa rasmi mabingwa wa Ligi Kuu, haitawafanya kuridhika, bali wanatafuta pointi zote tatu katika michezo iliyobaki ili kumaliza kwa heshima kubwa.

“Tunakutana na timu iliyopo chini, ipo katika wakati mgumu itakuja kucheza kwa kukamia kumfunga bingwa, lakini pamoja na kutafuta pointi muhimu zitakazowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo,” alisema kocha huyo.

Wakati Sven akihitaji heshima kwa sasa katika kutafuta pointi 12 katika michezo minne iliyobaki, chanzo chetu ndani ya klabu hiyo kimetueleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed 'Mo' Dewji, imeahidi kutoa kiasi cha Sh. milioni 400 za Kitanzania kwa wachezaji na benchi la ufundi baada ya kukunwa na kipigo ilichokitoa kwa watani zao, Yanga.

Kikosi cha Simba leo kitaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao dhidi ya Mbao FC utakaochezwa keshokuwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa