Simba kuwavaa mabingwa wa Morocco

03Aug 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba kuwavaa mabingwa wa Morocco

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya klabu ya Ittihad Riad de Tanger itakayofanyika leo Uturuki.

klabu ya Ittihad Riad de Tanger.

Mechi hiyo ya leo itajayofanyika kuanzia saa 10 jioni kwa saa za Tanzania ni ya pili kwa mabingwa hao baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya klabu nyingine kutoka Morocco.

Akizungumza jana jijini hapa, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema jana kuwa huo ni mwendelezo wa timu yao kupata mechi zitakazowaweka katika kiwango cha juu kuelekea msimu mpya.

Manara alisema kikosi chao kiko katika hali nzuri na benchi la ufundi linatarajia kuendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wake wengi kuonyesha uwezo wao.

"Tuko katika mipango ya kuhakikisha timu yetu inapata mechi ya tatu kabla ya kurejea, mwalimu anasema yeye anaziita hizo mechi ni sehemu ya mazoezi, na timu itarejea nchini Jumapili alfajiri," alisema kiongozi huyo.

Naye Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah alisema kuwa maandalizi ya Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 mwaka huu, yako katika hatua za mwisho na leo wanatarajia kumtangaza kiongozi ambaye atakuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo.

Abdallah alisema kuwa pia, klabu yake itatambulisha jezi mpya za klabu hiyo Jumapili pamoja wasanii ambao watatumbuiza katika Tamasha la Simba Day.Aliongeza kuwa katika mwendelezo wa wiki ya Simba, kesho wachezaji wakongwe wa timu hiyo watawatembelea wenzao wa Yanga katika malengo ya kudumisha umoja na ushirikiano kati ya klabu hizi mbili kongwe za hapa nchini.

Mabingwa hao wa Bara wamewaalika Asante Kotoko ya Ghana kucheza nao mechi ya kirafiki katika Tamasha la Simba Day.

Habari Kubwa