Simba, Lipuli hesabu kutawala Samora leo

15Feb 2020
Isaac Kijoti
Iringa
Nipashe
Simba, Lipuli hesabu kutawala Samora leo
  • ***Nonga aionya akimfukuzia Kagere kileleni mwa wafungaji bora, Sven asema...

WAKATI Simba ikitarajia kushuka katika Uwanja wa Samora mjini Iringa leo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao, Lipuli FC, wameonywa kwamba haitakuwa rahisi kuvuna alama tatu.

Simba yenye pointi 53 kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, itashuka dimbani ikipiga hesabu kali ya kuwania alama tatu ugenini kama ilivyofanya dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kuichapa mabao 3-0 kwenye mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Jamhuri, Jumanne wiki hii.

Kwa Lipuli itakuwa ikijiuliza kwa kuchanga karata zake vizuri kaada ya kushindwa kuutumia vema uwanja huo wa nyumbani katika mechi iliyopita kufuatia kulazimishwa sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania.

Hata hivyo, Simba itakuwa ikitaka kuendeleza ubabe wao wa mzunguko wa kwanza iliposhinda 4-0 ndani ya Uwanja wa Uhuru, shukrani kwa Meddie Kagere na Francis Kahata waliofunga bao moja moja na Hassan Dilunga aliyetupia mawili katika mchezo huo.

Lakini nahodha wa Lipuli FC, Paul Nonga, amesema watapambana kupata pointi tatu mbele ya Simba kwenye mchezo huo wa raundi ya 22 msimu huu.

Nonga ambaye ni kinara wa kucheka na nyavu katika klabu hiyo akiwa na mabao nane, manne nyuma ya straika wa Simba, Kagere anayeongoza kwenye msimamo wa wafungaji bora msimu huu, amesema itakuwa mechi ngumu lakini wamepania kuvuna alama tatu.

“Tunajua ligi msimu huu ni ngumu na kila timu inapambana kutafuta matokeo, hivyo tutakachokifanya ni kupambana na kujituma ili kupata alama tatu kutoka kwa wapinzani wetu," alisema na kuongeza.

“Tunatambua Simba ni timu kubwa ila inapofika uwanjani wote ni wachezaj, tumejipanga kuona tunapata matokeo.”

Huku wakikaribishwa na mvua jana katika mazoezi yao, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema anaamini wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo huo na anatarajia kupata matokeo.

Sven amesema anatambua haitakuwa mechi rahisi kutokana na timu nyingi kucheza kwa kujuhudi hususan zinapokuwa nyumbani dhidi ya Simba.

Alisema lakini anaamini wachezaji wake wataonyesha kiwango kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Kwa kiwango tulichokionyesha mechi iliyopita kama tutaendelea nacho ninaamini tunaweza kupata matokeo.

"Lengo letu ni kuendea kujiimarisha kileleni hadi tunatwaa ubingwa, na kila mchezaji analitambua hilo," alisema Sven ambaye amerithi mikoba ya Mbelgiji mwezake, Patrick Aussems.

Simba ipo keleleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 53, wakati Lipuli ipo nafasi ya tisa na pointi zake 29 baada ya timu hizo kila moja kushuka dimbani mara 21.

Habari Kubwa