Simba, Manara waachana rasmi

29Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Manara waachana rasmi
  • …Klabu yamshukuru kwa kazi aliyoifanya, huku nafasi yake ikipewa mwandishi wa habari…

KLABU ya Simba imetangaza kuachana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Haji Manara, baada ya kutotaka kuendelea kuhudumu klabu hiyo, na hapo hapo imemteua Ezekiel Kamwaga kuwa Kaimu Mkuu wa idara hiyo kwa muda wa miezi miwili.

Kwa mujibu ya taarifa iliyotolewa na klabu hiyo jana, ikitoka kwenye Bodi ya Wakurugenzi imesema kuwa imeridhia matakwa ya Manara kutoendelea kuhudumu katika nafasi hiyo kama Msemaji wa Klabu, hivyo imemshuruku na kumtakia kila la kheri katika shughuli zake.

Taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo, ilisema inamshukuru kwa maneno aliyoyatumia kuwaaga Wanasimba katika kundi la viongozi wa Simba (Simba HQ) na kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye klabu hiyo kwa kipindi chote alichoshika nafasi hiyo.

Katika taarifa hiyo, pia klabu hiyo imemteua Kamwaga kuwa kaimu kwa kipindi cha miezi miwili, ambacho atashiriki maboresho ya muundo na utendaji wa idara hiyo.

Ilisema kuwa kaimu huyo ni mwandishi wa habari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 kwenye tasnia ya habari, akifanya kazi kwenye vyombo vya habari vya ndani na kimataifa.

Pia, ilisema kuwa mkuu huyo anaijua vizuri klabu ya Simba na historia yake, kwani ameshawahi kuitumikia katika nafasi ya Msemaji na Kaimu Katibu Mkuu wa Simba.

Vile vile, taarifa hiyo ilisema mara baada ya maboresho ya Idara ya Habari na Mawasiliano, pamoja na idara zingine klabu itatangaza fursa mbalimbali za ajira katika kipindi cha wiki chache zijazo.

Manara aliteuliwa na klabu hiyo kuwa msemaji wa klabu 2015, akichukua nafasi ya Asha Muhaji aliyefariki mwaka 2020, na kuhudumu kwa miaka sita.

Kamwaga alishawahi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo 2014, kazi ambayo aliihudumu kwa muda wa miezi sita tu, chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa wakati huo, Ismail Aden Rage.

Ikumbukwe Kamwaga alichaguliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu akichukua nafasi ya Mwanasheria Evodius Mtawala, akitoka kuwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, na baada ya kuteuliwa, ndipo marehemu Muhaji naye akateuliwa kuchukua nafasi ya Kamwaga.