Simba: Mbabane hawatachomoka

28Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Mbabane hawatachomoka
  • ***Okwi arejea kuongoza mashambulizi katika mchezo huo....

IKIWA bila nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza, Simba inatarajia kuanza kibarua cha kusaka taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwakaribisha Mbabane Swallows kutoka Swaziland katika mechi ya kwanza ya ya hatua ya kwanza itakayochezwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini ....

mshambuliaji wa simba Emmanuel Okwi, picha na mtandao

Dar es Salaam.

Nyota wa Simba watakaokosekana katika mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Burundi ni pamoja na Shomari Kapombe, Asante Kwasi ambao ni majeruhi pamoja na Juuko Murshid ambaye ana matatizo ya kifamilia.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kocha wa makipa wa Simba, Mohamed Muharami, alisema kuwa kikosi chao kiko tayari kwa ajili ya kuwakabili Mbabane Swallows katika mchezo huo wa kimataifa na maandalizi ya mchezo huo yamekamilika.

Muharami alisema kuwa wanawaheshimu wapinzani wao lakini wamejiandaa kuanza vyema mashindano hayo ya kimataifa kwa sababu wanawawakilisha Watanzania na si klabu ya Simba pekee.

Kuelekea mchezo huo, mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi, amerejea katika hali yake ya kawaida na yuko tayari kuivaa Mbabane Swallows baada ya kuukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopita dhidi ya Lipuli FC.

Naye Kocha wa Mbabane Swallows, Kinnah Phiri, alisema kuwa wanafahamu walichokifata hapa nchini na anafurahi kuona amerejea Tanzania kwa mara nyingine.

"Tunashukuru tumefika salama, malengo yetu ni kufanya vizuri kesho (leo), tunajua kile tunachokitarajia, tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri, tunaifahamu pia Simba," alisema Phiri, ambaye aliwahi kuifundisha Mbeya City ya jijini Mbeya.

Waamuzi watakaochezea mechi hiyo ya leo ambao wanatoka Burundi ni pamoja na Pacifique Ndabihawenimana ambaye atasaidiwa na Willy Habimana na Gustave Baguma huku Georges Gatogato akiwa refa wa akiba na kamishna wa mchezo huo ni Mzambia, Joseph Nkole.

Simba itashuka katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bila kufungana na Lipuli FC wakati Mbabane Swallows wao walifungwa bao 1-0 na Malanti Chief.

Habari Kubwa