Simba, Mbabane tambo zatawala

27Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Mbabane tambo zatawala
  • ***Manara awaita mashabiki na kuwaahidi hawatawaangusha...

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, akisema timu yake itaingia na nguvu tofauti kuwakabili Mbabane Swallows kutoka Swaziland hapo kesho, wapinzani hao wamewasili nchini na kusema wako 'zaidi ya tayari' kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa simba Haji Manara, picha na mtandao

Aussems alisema kuwa kikosi chake kimejipanga kuanza vyema mashindano hayo lakini wakifahamu wanatakiwa kujituma na kucheza kwa kiwango cha juu.

Mbelgiji huyo alisema kuwa wachezaji wote wako tayari kwa mechi hiyo ya kwanza na wanataka kupata ushindi mnono ili kurahisha kazi watakaposafiri kwenda Mbabane kucheza mchezo wa marudiano.

"Tunafanya mazoezi magumu na mepesi, lengo letu ni kuwa imara kila idara, tunajua hakuna mechi rahisi, lakini mipango tuliyonayo ni kutumia vyema dakika 90 za uwanja wa nyumbani," alisema Aussems ambaye kesho ataiongoza Simba kwa mara ya kwanza katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema kuwa maandalizi ya mechi yao hiyo ya kimataifa yamekamilika na wanawataka mashabiki na wadau wa soka wasiwe na wasiwasi.

“Tunakwenda kuwakabili Mbabane keshokutwa (kesho) tukijua ni timu nzuri na ni mabingwa wenzetu, lakini tunajua matarajio ya Watanzania na Wanasimba kwetu, kiukweli hatutawaangusha na tunaahidi furaha kwenu," alisema Manara.

Kocha Msaidizi wa Mbabane Swallows, Thabo Vilakati 'Koki' alisema kuwa wamejiandaa vyema kuikabili Simba na kuwataka mashabiki wao wasiwe na hofu licha ya kufungwa bao 1-0 na Malanti Chief katika mchezo wa ligi uliochezwa Ijumaa iliyopita.

"Najua walisema mengi baada ya kufungwa, lakini hii ni sehemu ya mchezo, tuko zaidi ya tayari kwa ajili ya mechi hii ya mashindano ya Afrika," alisema Koki.

Wakati huo huo kikosi cha Mtibwa Sugar kinatarajia kuwakaribisha Northern Dynamo kutoka Shelisheli katika mechi ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa