Simba, Mbao nao wachemka

26Jan 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Mbao nao wachemka
  • ***Kombe na mamilioni ya SportPesa Cup yaenda Kenya kwa mara ya tatu mfululizo...

KOMBE la mashindano ya SportPesa litaenda Kenya kwa mara ya tatu mfululizo baada ya Bandari FC na Kariobang Sharks zote za nchini humo kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Beki wa Bandari, Bernard Odhiambo (kushoto), akipambana kumzuia mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya SportPesa iliyochezwa kwenye Uwanja vya Taifa jijini Dar es Salaam jana. Simba ilifungwa mabao 2-1. PICHA: HALIMA KAMBI

Bandari imetinga hatua hiyo baada ya kuwafunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliochezwa mapema mchana huku Mbao FC ya jijini Mwanza ikikubali kuchapwa penalti 6-5 na wababe wa Yanga, Kariobang Sharks kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili.

Wageni hao walilazimika kusubiri hadi hatua ya penalti baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika wakiwa sare ya bila kufungana.

Kwa matokeo hayo sasa, timu za Tanzania zilizobakia katika mashindano hayo, ambazo ni Simba na Mbao zitakutana katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu itakayotangulia kesho mchana.

Simba imeungana na watani zao Yanga kwa kuondoka mapema katika mashindano hayo yanayoandaliwa na wadhamini wao, Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana walipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo lakini makosa ya wachezaji wake yaliwagharimu na kujikuta wakifungwa na timu hiyo inayomilikiwa na Bandari ya Kenya.

Wenyeji hao walikuwa wa kwanza kufunga kupitia kwa Mnyarwanda, Meddie Kagere dakika ya 44 kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Hata hivyo tangu kuanza kwa mchezo, Bandari inayofundishwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Ben Mwalala walionekana kuwa watulivu na kuwasoma wapinzani wao.

Kipindi cha pili pamoja na Simba kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Juuko Mursheed, Hassan Dilunga na nafasi zao kuchukuliwa na Pascal Wawa na Emmanuel Okwi, bado walikosa umakini wa kuipita ngome ya Bandari.

Dakika ya 61, William Wadri aliisawazishia Bandari bao kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na Muzamiru Yassin ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Jonas Mkude kumchezea vibaya mshambuliaji wa Bandari ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru adhabu hiyo.

Simba iliendelea kumiliki mpira na kupanga mashambulizi lakini ubovu wa pasi za mwisho za viungo wake na mabeki wa pembeni ziliwanyima washambuliaji wake, Kagere na Okwi kukwamisha mpira wavuni.

Wakati Simba ikiendelea kuliandama lango la Bandari, walijikuta wakishambuliwa ghafla na kupelekea wageni kupata bao la pili dakika ya 78 lililowanyong'onyesha mashabiki wa Simba.

Matokeo hayo yameendelea kuwa mkosi kwa timu kongwe za Tanzania ambapo Simba na Yanga mara mbili mfululizo wameshuhudia Gor Mahia ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Habari Kubwa