Simba mdomoni kwa Esperance

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba mdomoni kwa Esperance
  • ***Nafuu kwake ni kwa Mamelodi, TP Mazembe, Aussems atoa sababu za ushindi huku...

KUJITUMA na kufuata maelekezo ndio moja ya sababu iliyoelezwa na Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, kufuatia ushindi wao wa mabao 2-1 kwenye mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita,-

KIKOSI CHA SIMBA SC.

ambapo sasa ipo katika nafasi ya kukutana na Mamelodi Sundowns, Esperance ama TP Mazembe.

Simba juzi iliibuka na ushindi huo, hivyo kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika, shukrani kwa mabao ya Mohammed Hussein 'Tshabalala' na Clatous Chama.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mchezo huo, Aussems alisema wapinzani wao walicheza soka zuri, lakini amewasifu wachezaji wake kwa kujituma na kufuata maelekezo yake kikamilifu.

"Lazima niwapongeze wachezaji wangu... wamefanya kile nilichowaelekeza..., tulihitaji ushindi kuweza kufuzu hatua ya robo fainali, wapinzani wetu walikuwa bora, lakini nafikiri sisi tulikuwa bora zaidi yao," alisema Aussems.

Alisema kila mmoja aliyepata nafasi ya kucheza juzi alipambana kwa ajili ya timu.

"Na hata mabadiliko niliyoyafanya yalikuwa ya kiufundi, lengo lilikuwa kushambulia zaidi baada ya kuwa tupo nyuma kwa bao moja," alisema Aussems.

Kwa ushindi huo wa juzi, Simba inakuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufuzu hatua ya robo fainali tangu michuano hiyo ianze kuendeshwa kwa mfumo mpya mwaka 1997 na inaungana na All Ahly kufuzu hatua hiyo kutoka Kundi D lililokuwa likiijumuisha pia JS Saoura iliyomaliza nafasi ya tatu.

 

Robo Fainali

Simba ambayo imemaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa nyuma ya Al Ahly yenye alama 10, sasa inasubiri droo itakayochezeshwa Jumatano Cairo, Misri kujua mpinzani wake ajaye.

Kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) linalosimamia michuano hiyo, Simba itakutana na moja ya timu iliyoongoza makundi mengine matatu na si kutoka katika kundi lake, Al Ahly.

Kwa mantiki hiyo Simba inaweza kukutana na kinara wa Kundi A, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ama bingwa mtetezi aliyeongoza Kundi B, Esperance ya Tunisia au kuangukia kwa TP Mazembe ya DR Congo kutoka Kundi C.

Timu zinazoweza kukutana na Al Ahly ni zilizoshika nafasi ya pili katika makundi mengine ambazo ni Wydad Casablanca ya Morocco kutoka Kundi A au Horoya ya Guinea kutoka Kundi B ama Constantine ya Algeria iliyokuwa Kundi C.

Hatua ya robo fainali mechi hizo zitaanza kuchezwa kati ya Aprili 6 na 7, huku mechi za marudiano zikitarajiwa kupigwa Aprili 13 na 14, mwaka huu.

Habari Kubwa