Simba: Miquissone atazalisha vishindo

05Aug 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Miquissone atazalisha vishindo

KOCHA na mchezaji wa zamani wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Talib Hilal, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kumruhusu nyota wake, Luis Miquissone kujiunga na Al Ahly ya Misri kwa sababu ya dau nono la Dola za Marekani 900,000 ambazo wameweka mezani.

Tayari Simba imemtambulisha kiungo mpya, Peter Banda aliyesaini mkataba wa miaka mitatu na kutajwa huenda akawa ni mrithi wa Miquissone.

Talib alisema dau hilo ni kubwa na Simba inatakiwa kufahamu mpira ni pesa na ofa hiyo iliyotolewa na mabingwa hao wa Afrika ni nzuri na inaweza kusaidia kununua wachezaji wengine watatu wazuri kutoka nje ya Tanzania.

Alisema sasa ni wakati wa Simba kuwa makini kufanya biashara kwa sababu ana imani kwamba nyota huyo atawafungulia milango wengine na kuhakikisha wanapopata fedha hizo wanasajili wachezaji wengine watakaoziba mapengo mapema.

"Simba hawana sababu ya kuchelewesha ofa hiyo kwa kuangalia faida kwa klabu, pia nzuri hata kwa mchezaji mwenyewe kujaribu bahati yake kwingine, mbona TP Mazembe walimuuza Mbwana Samata na alikua ndio mfungaji wao pekee,".

"Usajili wa Peter Banda kwangu ni mchezaji mzuri na ndio mrithi sahihi wa Miquissone, ana uwezo na kiwango cha kucheza vizuri na ataisaidia Simba kufikia malengo yake," alisema Talib.

Naye Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alisema wataweka wazi baada ya mchakato wa usajili wa Miquissone utakapokamilika kwa sababu bado uamuzi wa kuondoka au kubakia Simba haujakamilika.

“Tumewekeza zaidi kwa upande wa wachezaji ili kuwa na kikosi bora, mashabiki wawe na subira, mambo mazuri yataonekana katika eneo hilo kwa kupata wachezaji bora kulingana na mapungufu yetu ambayo yalionekana msimu uliomalizika, tutakuwa na kishindo," alisema Mangungu.