Simba mlangoni kwa Yanga

20Feb 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba mlangoni kwa Yanga
  • ***Ni baada ya Morrison kuwakera Biashara United kwa kuipa pointi tatu huku...

KWA mara nyingine tena, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, wameendeleza rekodi safi ikicheza kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara dhidi ya Biashara United, ilipopata ushindi wa bao 1-0 kwenye mfululizo wa ligi hiyo, hivyo kuwapigia hodi watani zao, Yanga waliopo kileleni.

Hii ni mara ya tatu kwa mabingwa hao kupata ushindi tangu timu hiyo ya Biashara United ipande na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2018/19, ambapo ilifungwa mabao 2-0 Aprili 27, 2019, yakifungwa na John Bocco, na Septemba 29, 2019, msimu wa 2019/20, yakifungwa na Meddie Kagere na Miraji Athumani.

Alikuwa ni Bernard Morrison aliyepeleka pointi zote tatu Msimbazi, alipofunga bao hilo pekee dakika ya 21, ambalo limeifanya Simba kufikisha pointi 42 katika nafasi ya pili baada ya mechi 18, hivyo kuikaribia Yanga mlangoni ambayo ipo kileleni ikiwa na alama 46 zilizotokana na michezo 20.

Kwa msimamo huo jinsi ulivyo, endapo Simba itashinda mechi zake za viporo, itafikisha pointi 48, hivyo kuwapiku watani zao kwa alama mbili zaidi.

Bao hilo lilitokana na kizaazaa kilichotokea kwenye lango la Biashara United, Thadeo Lwanga akipiga shuti lililookolewa na mguu na kipa James Ssetuba, lakini ukarudisha tena kwenye eneo la hatari na kumkuta Hamis Ndemla aliyemmegea pande Morrison akiwa yeye na kipa, akaujaza wavuni kwa shuti dhaifu la kiufundi.

Linakuwa ni bao la tatu la Morrison msimu huu, akijiunga na Simba kutokea Yanga, Februari 4, mwaka huu akifunga bao la ushindi kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma dhidi ya Dodoma Jiji, Simba ikishida 2-1, bao lake la kwanza akifunga Novemba 21, mwaka jana kwenye mechi ambayo Simba ilishinda mabao 7-0 dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Mchezaji aliyesajiwa kipindi cha dirisha dogo akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, Perfect Chikwende alikosa bao la wazi, akiwa anatazama na kipa Ssetuba, lakini alipiga shuti lililopaa juu dakika ya 44 ya mchezo.

Kipindi cha pili timu ziliendelea kucheza mchezo kama wa kipindi cha kwanza, wa kutumia nguvu na mipira mirefu kutokana na hali ya uwanja iliyokuwa na nyasi ndefu, pasi fupi zikikwama kufikia walengwa.

Dakika ya 50, Aishi Manula aliruka mbizi kuuokoa mpira wa krosi iliyokuwa inakwenda kutua kwenye kichwa cha Deogratius Judika, lakini mpira huo ulimkuta Mghana Christina Zigah akapiga shuti lililotoka nje kidogo ya lango.

Habari Kubwa