Simba: Moto huu tutauzimia Songea

14May 2018
Isaac Kijoti
SINGIDA
Nipashe
Simba: Moto huu tutauzimia Songea
  • ***Sherehe za ubingwa zaanzia Dodoma, ikitinga mjengoni leo...

BAADA ya kuituliza Singida United kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa Namfua juzi, Simba imesema moto wa ushindi waliouwasha tangu kuanza kwa ligi hiyo hautazimwa hadi watakapohitimisha mechi mbili zilizobaki.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, imebakiza mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa Uwanja wa Taifa wiki hii na kisha kuifuata Majimaji ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizunguza na Nipashe mara baada Shomary Kapombe kuipa Simba ushindi wa bao hilo pekee, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma, alisema lengo lao ni kumaliza bila kupoteza.

Alisema kila baada ya mechi kumalizika, maandalizi ya mchezo unaofuata yanafanyika kama kawaida bila kujali kuwa wameshatwaa ubingwa.

"Hatubweteki na kutwaa ubingwa mapema, lengo letu ni kuona tunaweka rekodi ya kutopoteza mechi hadi ligi inamalizika.

"Hivyo maandalizi yetu yanaendelea, kama vile hatujatwaa ubingwa, sasa tunaiwazia Kagera Sugar na kisha Majimaji," alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Akizungumzia mechi hizi za lala salama ikiwamo ya juzi wapinzani wao kuwakamia, Djuma alisema kikosi chao hutumia makosa madogo yanayofanywa na wapinzani ili kuibuka na ushindi.

"Lengo kwetu ni pointi tatu na kama nilivyosema tunajiandaa kila baada ya mechi, ndiyo maana unaona mwisho wa siku tunashinda," alisema.

Kwa upande wa Afisa Habari wa Simba, Hajji Manara, alisema ushindi huo unaonyesha Simba ni mabingwa waliostahili.

Alisema sherehe za ubingwa Simba zimeanza na jana waliandaliwa hafla ya kupongezwa na wabunge mashabiki wa timu hiyo jijini Dodoma.

Manara alisema mara baada ya hafla hiyo leo, Jumatatu kikosi cha mabingwa hao kitatinga bungeni kwa mwaliko wa wabunge hao.

Simba ambayo tayari ni mabingwa wa ligi hiyo, jana walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Combine ya Dodoma wakati huu ikijiandaa kuivaa Kagera Sugar wiki hii.