Simba, Namungo zafunguka fainali

01Aug 2020
Somoe Ng'itu
Rukwa
Nipashe
Simba, Namungo zafunguka fainali

TUKO tayari! Hayo ni maneno kutoka katika benchi la ufundi la Simba ya jijini Dar es Salaam kuelekea mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Namungo FC ya Lindi itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga.

Simba ilitinga fainali ya mashindano hayo baada ya kuwafunga Azam FC katika mechi ya hatua ya robo fainali na baadaye kuwaondoa Yanga kwenye hatua iliyofuata kwa kuwapa kichapo cha mabao 4-1.

Wekundu wa Msimbazi wataingia uwanjani leo huku wakiwa na kumbukumbu ya kushinda Ngao ya Jamii na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema wanahitaji kumaliza fainali hiyo 'mapema' ili kukamilisha malengo yao ya kutwaa kikombe cha tatu msimu huu na cha pili chini ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck.

Matola alisema wachezaji na benchi la ufundi wako tayari na mchezo huo ambao hautakuwa na presha kubwa kwa sababu tayari timu zote mbili (Simba na Namungo), zimeshakata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.

"Tulifika Sumbawanga tangu jana (juzi) jioni, na leo (jana) jioni tutafanya mazoezi mepesi ya mwisho, kila mchezaji anajua tunahitaji kurudi na ushindi, ingawa tumewaambia Namungo ni timu nzuri na yenye wachezaji wenye kasi, tunahitaji kuthibitisha ubora wetu wa msimu mzima," alisema Matola.

Aliongeza hakuna mchezaji majeruhi na alimtaja nyota Tairone Santos ndiye aliachwa Dar es Salaam kwa sababu bado hajawa fiti tangu alipoumia katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo iliyochezwa mapema mwezi uliopita.

Naye Kocha Mkuu wa Namungo, Thierry Hitimana, alisema kikosi chake kimejiandaa kukutana na ushindani kwa sababu watacheza dhidi ya timu bora na yenye wachezaji wenye uzoefu wa mechi za michuano mbalimbali.

"Ni mechi kubwa, lakini fainali huwa haina mwenyewe, ukitumia vema nafasi na kujaribu kupunguza makosa, una nafasi nzuri ya kupata ushindi, tunamuomba pia Mungu awe upande wetu, tunahitaji kushinda na kupata kikombe hiki cha kwanza msimu huu," alisema Hitimana.

Aliwataja wachezaji wake waliokuwa majeruhi akiwamo Blaise Bigirimana na Reliant Lusajo wameimarika na atawatumia katika fainali hiyo ambayo kwa timu yake ni mafanikio makubwa.

Habari Kubwa