Simba ni “Do or Die

16Mar 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba ni “Do or Die
  • ”

***Inahitaji ushindi tu ili kutinga hatua ya robo fainali baada...
USHINDI, Ushindi, ushindi! Hayo ndiyo malengo ya Simba ambayo inatarajia kuikaribisha AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mechi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems, picha mtandao


Mechi hiyo ya Kundi D itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku sawa na mchezo mwingine wa kundi hilo utakaowakutanisha Al Ahly ya Misri dhidi ya JS Saoura ya Algeria.


Simba ilianza safari ya kutinga hatua ya robo fainali kwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-0, halafu ikaenda kufungwa mabao 5-0 huko DRC na kupokea kichapo kingine kama hicho na Al Ahly halafu ikaja kuwafunga Waarabu hao wa Misri bao 1-0.


Baada ya mchezo huo, Simba wawakilishi pekee wa Afrika Mashariki na Kati waliobakia katika mchezo huo wakapoteza mchezo watatu wa ugenini kwa kufungwa mabao 2-0 na JS Saoura na kuwafanya waburuze mkia kwenye kundi lao wakiwa na pointi sita.


Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems, aliliambia gazeti hili jana kuwa wamefanya mazoezi ya nguvu na kikosi chake kiko tayari kuelekea mchezo huo ambao wanahitaji ushindi tu ili waweze kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka barani Afrika.


Aussems alisema kila mchezaji wa timu hiyo anataka kuwa sehemu ya mafanikio kwa kuhakikisha wanashinda na kucheza hatua ya robo fainali ambayo hawajacheza kwa miaka 16 sasa.


"Tuko tayari na tutafanya kila linalowezekana ili kupata matokeo chanya, tutapokea chochote kile ambacho kitatokea, huu ni mpira," alisema Mbelgiji huyo.
"Kufanya vizuri kwetu tutaifanya Tanzania iweze kutangazika... kwa pamoja, tunaahidi tutapambana, tutapigana kuhakikisha tunafanya vizuri, kama ilivyo kauli mbiu yetu ni Do or Die," alisema kipa huyo chaguo la kwanza la Simba.


Naye Kocha Mkuu wa AS Vita, Florente Ibenge, alisema mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu, yenye ushindani na ni fainali kwa kila upande.


"Tumekuja hapa kwa ajili ya kusaka ushindi, tunajua atakayeshinda atakuwa amesonga mbele, tunataka kushinda ili tuendelee katika mashindano haya," alisema Ibenge ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya DRC.KAGERE VS MAKUSU


Mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara akishirikiana na Mganda, Emmanuel Okwi pamoja na nahodha, John Bocco.


Kagere ndiye anaongoza kwa kupachika mabao katika michuano hiyo akiwa na magoli sita.
Jean Marc Makusu, nyota wa AS Vita amefunga mabao matano kwenye michuano hiyo msimu huu na anatakiwa kuchungwa na mabeki wa Simba ili asiweze kuziona nyavu katika mechi ya leo.


Kikosi cha AS Vita ambacho kimetua nchini, kina wachezaji wawili tu kutoka nje ya DRC ambao ni golikipa Mcameroon, Nelson Lukong na beki wa kati, Savio Kabugo. Habari Kubwa