Simba: Njooni Al Ahly hatoki

22Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Njooni Al Ahly hatoki
  • ***Mo Dewji atinga mazoezini kwa Mkapa na viongozi wote, ulinzi waimarishwa, Gomes asema...

LICHA ya kueleza kuwa wanawaheshimu mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly, miamba ya soka nchini, Simba imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho kwa kuwa wamejipanga kuilinda rekodi yao.

Simba itaikaribisha Al Ahly kesho katika uwanja huo kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza katika michuano ya kimataifa ikiwa nyumbani kwa zaidi ya miaka sita.

Timu hizo ambazo zipo Kundi A, kila moja itataka kuendeleza ushindi wake baada ya kuanza kwa kushinda ambapo Simba ikiwa ugenini ilichapa Klabu ya AS Vita ya DR Congo bao 1-0 wakati Al Ahly wakiwa nyumbani waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan.

Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes Da Rosa, amesema anawaheshimu sana Al Ahly, lakini morali wa wachezaji wake ipo juu na kila mmoja ana kiu ya kupambana kwenye mchezo huo ili kuendeleza ushindi walioupata dhidi ya AS Vita.

Gomes alisema wapo kundi gumu lenye ushindani mkali na ushindi wao walioupata dhidi ya AS Vita umeongeza nguvu kwao ya kupambana, lakini wanatambua Al Ahly nayo inataka kuendeleza ushindi walioupata dhidi ya Al-Merrikh, hivyo haitakuwa mechi rahisi.

"Mchezo utakuwa mgumu ila tupo tayari na tunawaheshimu wapinzani wetu, kikubwa ni kwamba tutaingia ndani ya uwanja kwa tahadhari kwa kuwa Al Ahly ni timu nzuri ila ushindi wetu dhidi ya AS Vita umeongeza nguvu na morali kwa wachezaji," alisema Gomes ambaye amerithi mikoba ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck.

Kwa upande wa Kocha wa Al Ahly,  Pitso Mosimane, baada ya kutua nchini Ijumaa alitabiri mchezo huo kuwa mgumu, lakini akieleza pengine wanaweza kusahihisha makosa yao waliyoyafanya walipokubali kichapo cha bao 1-0 mwaka 2019 timu hizo zilipokutana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam katika hatua hiyo.

“Tumejiandaa vizuri kuivaa Simba, utakuwa mchezo mgumu, Simba ilitufunga mara ya mwisho tulipokutana hapa, hivyo labda itakuwa wakati wetu wa kusahihisha hilo,” Mosimane aliliambia Nipashe.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, wamewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwa kuwa timu yao imefanya maandalizi makubwa ya kuhakikisha inapata matokeo husuan ikiwa nyumbani.

Manara alisema haipendezi kwa shabiki wa Simba aliyeko jijini Dar es Salaam kuikosa mechi hiyo ambayo wameipa kaulimbiu ya "Total War" (Vita Kamili), ikichagizwa na "The Point of No Return" (Hakuna Kurudi Nyuma).

Wakati huo jana katika mazoezi ya Simba yaliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, viongozi wote wa ngazi za juu akiwamo Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba , Mohamed "Mo" Dewji, walihudhuria na kuteta na wachezaji huku pakiwa na ulinzi mkali, lakini pia wanahabari wakizuiwa kuingia kushuhudia mazoezi hayo.

Habari Kubwa