Simba pungufu kuikabili Lyon

06Oct 2018
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba pungufu kuikabili Lyon
  • ***Tetesi za kutimuliwa kocha msaidizi wake zarejea tena...

HUKU tetesi za kufukuzwa kwa Kocha Msaidizi wa timu yake zikiwa zinaendelea kusambaa, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatarajia kuwakaribisha African Lyon katika mechi ya ligi hiyo inayotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba iliyocheza mechi sita inashuka uwanjani ikiwa na pointi 11 wakati African Lyon iliyorejea kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi nane.

Katika mechi ya leo, Simba itaendelea kumkosa nahodha wake, John Bocco, ambaye amefungiwa mechi tatu kutokana na kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Mwadui wakati timu hizo zilipokutana pamoja na Hassan Dilunga na Asante Kwasi ambao ni majeruhi.

Hata hivyo hadi katika mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mchezo huo ya jana jioni, nyota wanne walioko kikosi hicho cha Simba cha timu ya Taifa (Taifa Stars) ambao ni Aishi Manula, Jonas Mkude, Shomary Kapombe na Bocco walikuwa hawajarejea kwenye klabu yao.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo yameendelea vizuri licha ya kuwapo na programu ya timu ya Taifa (Taifa Stars) kuingilia kati.

Aussems alisema kuwa anaamini wachezaji wake watakaopata nafasi ya kucheza mechi hiyo wataendelea kupambana ili kusaka matokeo mazuri.

DJUMA: SIHOFII KUFUKUZWA

Uongozi wa klabu hiyo jana ulikutana na Djuma na moja ya mazungumzo yanayodaiwa ni ya kuvunja mkataba na kocha huyo raia wa Burundi.

"Ni kweli nimeitwa na Rais (Salim Abdallah), ila kwa upande wangu tuko tayari kupokea uamuzi wowote watakaouchukua, riziki ni popote, haipatikani Simba peke yake, kiukweli ninashangazwa sana na maneno ambayo yamekuwa yanazungumzwa juu yangu, Mungu ndio anajua," alisema Djuma.

Mechi nyingine za Ligi Kuu Bara zitakazochezwa leo ni kati ya Singida United dhidi ya Ndanda, Kagera Sugar itawakaribisha Ruvu Shooting wakati Prisons itawavaa Mbeya City na KMC itawafuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.

Habari Kubwa