Simba Queens kibaruani Iringa

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba Queens kibaruani Iringa

TIMU ya Simba Queens ya jijini Dar es Salaam inatarajia kushuka dimbani kucheza mechi yake ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania dhidi ya wenyeji Panama Queens, itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa.

SIMBA QUEENS

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan "Mgosi" amesema kikosi chake kimekwenda Iringa kwa kazi moja ya kusaka pointi tatu muhimu na si matokeo mengine.

 

Mgosi alisema ameshazungumza na wachezaji wake na kuyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mechi iliyopita, na sasa anaamini wataingia uwanjani kwa lengo la kutekeleza mafundisho yake.

 

"Ligi ina ushindani na ina changamoto mbalimbali, ila tumekuja hapa (Iringa) kwa ajili ya kufuata pointi tatu, kila mchezaji anajua umuhimu wa mechi hii, hatutaki kupoteza tena pointi," alisema Mgosi, mshambuliaji wa zamani wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba.

 

Naye nahodha wa timu hiyo, Mwanahamisi Omary 'Gaucho', aliliambia gazeti hili kuwa ushindani katika ligi hiyo msimu huu umeongezeka, lakini anaamini watafanya vizuri zaidi.

 

"Wachezaji tunajuana, ndio maana ligi inazidi kuwa ngumu, ila tutaendelea kupambana," alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo aliyetua Simba Queens akitokea Mlandizi Queens.

 

Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya Marsh Academy dhidi ya JKT Queens, Alliance Girls vs Baobab Queens, Sisterz FC dhidi ya Tanzanite SC, Evergreen Queens dhidi ya Mlandizi Queens.

Habari Kubwa