Simba Queens, Ruvuma hapatoshi

29Jun 2020
Somoe Ng'itu
Mbeya
Nipashe
Simba Queens, Ruvuma hapatoshi

TIMU ya Simba Queens kutoka Dar es Salaam inatarajia kuwakabili wenyeji Ruvuma Queens katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Ligi hiyo imerejea tena baada ya kusimama tangu Machi, mwaka huu kutokana na kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona.

Kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' alisema wamejiandaa kupambana katika mchezo huo ambao utakuwa na ushindani kutokana na ubora wa timu zote mbili.

Mgosi alisema amewaandaa wachezaji wake kuwaheshimu wapinzani wao ili watimize malengo yao ya kuondoka na pointi tatu muhimu za kuwaimarisha kwenye mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.

Alisema kikosi chake kiliwasili salama mjini Songea na wako tayari kwa mchezo huo wa kwanza tangu kutokea kwa janga la corona ambalo lilisimamisha ligi na shughuli mbalimbali duniani.

"Tunataka kuanza nao, ndio ni timu nzuri, lakini nakumbuka wanakutana na Simba Queens, malengo yetu ni ubingwa, tunataka kushinda mechi tatu za kwanza za ugenini, hapo tutakuwa tumejiweka pazuri, halafu mikakati itaendelea tukirudi Dar es Salaam," alitamba kiungo huyo wa zamani wa Simba.

Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya Marsh Queens dhidi ya TSC Queens kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza wakati Panama Queens itawakaribisha Mlandizi Queens kwenye Uwanja wa CCM Samora mkoani Iringa

Habari Kubwa